Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa: Jihadi ni nguzo muhimu na yenye kuleta mabadiliko katika dini ya Kiislamu ambayo inatilia mkazo ushirikiano na Muqawama wa pamoja katika kupambana na dhulma mbali na kuhimiza jitihada za mtu mmoja mmoja.

Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabi Fard, amesema hayo kwenye khutba za leo za Sala ya Ijumaa iliyosaliwa kwenye viwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran na kuongeza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuhimiza kuwa wanyenyekevu, wapole katika matamshi, wenye maadili na tabia njema, tuheshimu haki za binadamu na kupigania haki daima lakini pia tusikubali kudhulumiwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika Qurani Tukufu: Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa – na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran pia amesema: Dini ya Kiislamu inaipa heshimna maalumu jamii ya wanadamu, inalenga kuleta mabadiliko katika jamii ya wanadamu na inazingatia ubora wa kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kiulinzi. Jihadi ina nafasi ya kipekee na maalumu katika dini hii, na neno jihadi na minyambuliko yake limetajwa mara 35 katika Qur’ani Tukufu.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema: Mzizi wa neno hili ni juhd lenye maana ya kufanya juhudi na jitihada kubwa zaidi za kufikia lengo. Katika muundo wa lugha ya Kiarabu linaashiria aina ya ushirikiano, makabiliano na ushindani baina ya makundi. 

Hujjatul Islam Abu Turabi Fard ameongeza kuwa: Unapoiangalia historia ya maisha ya kijamii na kisiasa ya mwanadamu utaona kwamba vita ni jambo lisiloepukika, lakini Qur’ani inaelekeza watu wasiingie vitani isipokuwa kwa kujihami, kupambana na uasi, wachupaji mipaka na wanaodhulumu haki za wengine. Jamii ya Kiislamu lazima isimame imara kupambana kijihadi na kujihami mbele ya wale wote wanaowasha moto wa vita dhidi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *