Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani amekutana na Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Moscow, na kumkabidhi ujumbe wa moja kwa moja kutoka kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Tovuti ya habari ya Press TV imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Dakta Larijani, ambaye pia ni mshauri wa Kiongozi Muadhamu, alisafiri kwenda Russia Alkhamisi asubuhi.

Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali, yakiwemo mahusiano baina ya nchi hizi mbili, ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya kikanda na masuala ya kimataifa.

Wiki iliyopita, Putin alisema kuwa viongozi wa Israel wamemtaka awasilishe ujumbe kwa Iran kwamba hawatafuti makabiliano na vita zaidi na Iran na wanataka kupunguza mvutano.

“Tunaendelea na mawasiliano ya kujiamini na Israel na tunapokea ishara kutoka kwa uongozi wa Israel ukiomba kwamba hili lifahamishwe kwa marafiki zetu wa Iran, kuwa Israel inakusudia na imedhamiria kutatua suala hilo zaidi, na haipendezwi na aina yoyote ya makabiliano,” alisema Putin akihutubia mkutano wa kilele wa Asia ya Kati na Russia huko Dushanbe Alkhamisi ya wiki iliyopita

Mvutano kati ya Iran na Israel uliongezeka baada ya utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds kuanzisha uchokozi usio na msingi dhidi ya Iran mnamo Juni 13, na kupelekea kuibuka vita vya siku 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *