Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kujenga Hospitali kubwa ya mama na mtoto mkoani Dodoma ikiwa kitashinda uchaguzi mkuu ujao.

Ahadi hiyo imetolewa na mgombea mwenza wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi leo Ijumaa Oktoba 17, 2025 wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Nkuhungu Jimbo la Dodoma Mjini.

Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM kwa kuona umuhimu wa Dodoma, imeamua kuwa itajenga hospitali hiyo na kukarabati Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ili iwe kituo cha mafunzo kwa watu wa ndani na nje ya nchi.

Kwenye maboresho hayo, amesema yataigusa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambayo mbali na kufanyiwa maboresho lakini itaongezewa uwezo wa vifaa vya kisasa.

“Lakini tunakwenda kujenga maktaba kubwa ya kisasa ambayo itakuwa na kila kitu, itahifadhi maandiko na wasomi watapata nafasi ya kufanya tafiti zao hapo,” amesema Dk Nchimbi.

Hata hivyo amesema yote yatawezekana ikiwa Taifa litaendelea kubaki katika amani na utulivu ambavyo huzaa usalama na maendeleo.

Mgombea mwenza ameomba wananchi kumchagua mgombea wa CCM Samia Suluhu Hassan kwani amejipambanua katika kipindi cha miaka minne aliyoongoza Taifa ameonekana kuwa mtu mwenye uwezo wa kukabidhiwa nchi.

Ametaja moja ya uimara wa Samia ni kwenye udhibiti wa mfumuko wa bei ambao haupandi ukilinganisha na mataifa mengine ambayo amesema kila kukicha bidhaa zinapanda bei.

Katika hatua nyingine Dk Nchimbi amesema hivi sasa Tanzania inapokea wawekezaji wakubwa 901 kwa mwaka tofauti na miaka minne nyuma ambapo ilikuwa ikipokea 207 kwa kipindi kama hicho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kukichagua CCM ambacho amesema ngome yake ni mkoa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *