Donald Trump ametangaza siku ya Alhamisi, Oktoba 16, kwamba atakutana na Vladimir Putin huko Budapest, mji mkuu wa Hungary, bila kutoa tarehe maalum, baada ya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Urusi ambapo amehakikisha kwamba “mafanikio makubwa yamepatikana.” Ikulu ya White House na Kremlin zimeripoti mkutano “mzuri na ambao umekuwa wenye matunda”. Mkutano huo umekuja siku moja kabla ya ziara ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Washington.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu mjini Washington, Vincent Souriau

Donald Trump ameelezea mazungumzo “yenye tija” na Vladimir Putin, wakati usitishaji wa mapigano kati ya Israel na Hamas ulijadiliwa. Rais Putin, Donald Trump ameandika, “amenipongeza kwa hatua hii nzuri ya kuleta amani.” “Na ninaamini,” rais wa Marekani ameongeza, “kwamba mafanikio haya yatatusaidia kupata njia ya kuondokana na vita kati ya Urusi na Ukraine.” 

“Nimemaliza tu mazungumzo yangu ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin, na yalikuwa na tija kubwa. Rais Putin alinipongeza mimi na Marekani kwa mafanikio haya makubwa ya amani katika Mashariki ya Kati, jambo ambalo amesema tumekuwa tukiliota kwa karne nyingi. Kwa kweli ninaamini kwamba mafanikio katika Mashariki ya Kati yatatusaidia katika mazungumzo yetu ya kumaliza vita na Urusi na Ukraine,” rais huyo wa Marekani ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Truth Social.

Donald Trump amesema kulikuwa na majadiliano mengi kuhusu uhusiano wa kibiashara kati ya Moscow na Washington, na jinsi uhusiano huu unaweza kubadilika ikiwa mzozo wa Ukraine utamalizika. Viongozi hao wawili walikubaliana kukutana mjini Budapest, Hungary. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika “ndani ya wiki mbili zijazo,” Trump amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.

Huu utakuwa mkutano wao wa pili wa ana kwa ana kuhusu vita nchini Ukraine, kufuatia mkutano wa kilele wa mwezi Agosti huko Alaska, ambao haukuzaa matunda yoyote. Kwa upande wa Marekani, akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, Donald Trump ameonyesha kwamba angejadili masuala yote haya na Volodymyr Zelensky, rais wa Ukraine anayetarajiwa katika Ikulu ya White House leo Ijumaa. “Ninaamini,” Donald Trump amehitimisha, “kwamba tulifanya maendeleo makubwa wakati wa mazungumzo haya ya simu.”

“Kufuatia wito huo, tulikubaliana kuwa kutakuwa na mkutano wa washauri wetu wakuu wiki ijayo. Mikutano ya awali kutoka Marekani itaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, pamoja na watu wengine mbalimbali watakaoteuliwa. Mahali pa kukutana panafaa kuamuliwa. Kisha mimi na Rais Putin tutakutana katika eneo tulilokubaliana, Budapest, Hungary, kuona kama tunaweza kukomesha vita hivi kati ya Urusi na Ukraine.” Rais Zelensky na mimi tutakutana Ijumaa katika Ofisi ya Oval, ambapo tutajadili mazungumzo yangu na Rais Putin, na mengi zaidi. Ninaamini maendeleo makubwa yamepatikana kutokana na mazungumzo ya simu ya leo,” ameandika kwenye jukwaa lake la Truth Social.

Kremlin inasema inafanya kazi kuandaa mkutano wa kilele

Kremlin imebainisa siku ya Alhamisi jioni kwamba inafanya kazi kuandaa mkutano huu mpya, kufuatia mazungumzo ya simu ya “karibu saa mbili na nusu” kati ya wawili hao katika mpango wa Moscow. Rais wa Urusi ameelezea mazungumzo hayo kuwa “ya wazi kabisa na ya uaminifu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *