Dar es Salaam. Msanii  wa Bongo Fleva, Queen Darleen, amezungumzia ukimya wake wa muda mrefu bila kutoa wimbo wowote akisema hajafulia na kwamba ndoa sio chanzo cha kusimama muziki wake kama watu wanavyoongelea.

Akipiga stori na Mwananchi, Queen Darleen ambaye amewahi kutamba na nyimbo kama Kijuso, Touch, Tawile na nyingine amesema shughuli za ujasiriamali anazozifanya ndizo zilizomfanya akapotea katika gemu ya muziki.

“Mimi bado ni mwanamuziki, ndoa wala haijanisababishia kuacha muziki, ipo siku nitarudi upya kama nilivyokuwa zamani, hivyo mashabiki wangu wawe wavumilivu tu,” amesema.

Muimbaji huyo anayefahamika kuwa chini ya lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ya Diamond Platnumz, alifunga ndoa mwaka 2019 na mfanyabiashara maarufu Isihaka Mtoro na kupata mtoto wa kike kwenye ndoa hiyo, ila kabla ya kuingia kwenye ndoa alikuwa na mtoto mwingine wa kiume.

Katika ndoa hiyo, Queen Darleen aliolewa mke wa pili na kulikuwa na madai ya kutoelewana na mke mwenzake, lakini katika hili amesema hayuko tayari kulizungumzia akisema ndoa ni mambo yake binafsi.

“Ukweli si unaona sijawahi kuzungumzia popote kuhusu ndoa yangu, basi kwenye hili niache kwanza, maana napenda kuweka siri mambo yangu ya familia,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *