Makamu wa Rais Kithure Kindiki ametangaza kuwa ibada ya mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga yatafanyika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo siku ya Ijumaa, kuanzia saa 9 asubuhi na yatadumu kwa saa mbili.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kindiki, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya mazishi ya kitaifa ya Raila Odinga, amesema hafla hiyo itajumuisha heshima za kijeshi, mahubiri ya kidini yatakayotolewa na Kanisa la Anglikana la Kenya, maombi kutoka kwa familia, na heshima kutoka kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa.

“Kamati inawashukuru maelfu ya watu wanaoendelea kumuomboleza kwa heshima na kutoa wito wa utulivu na kuheshimu sheria wakati kipindi cha maombolezo kinaingia siku yake ya pili kesho,” Kindiki ametangaza katika makazi yake Karen siku ya Alhamisi.

Wakenya hususan wale wanaoishi Mjini Nairobi hii leo siku ya Ijumaa watapata fursa ya kuuaga mwili wa Raila Odinga kwa siku ya pili mfululizo katika uwanja wa Nyanyo Jijini Nairobi.

Makamu wa Rais amebainisha kuwa kuagwa kwa mwili wa Raila kutaendelea baada ya hafla ya serikali, ambayo inaweza kuendelea hadi alasiri, ili kuruhusu Wakenya zaidi kutoa heshima zao za mwisho.

Makamu wa Rais alithibitisha kuwa viongozi kadhaa wa kigeni na wakuu wa nchi tayari wamethibitisha kuhudhuria hafla hiyo ya ibada ya mazishi.

Familia na serikali tangu wakati huo zimetoa wito wa utulivu na utu katika kipindi chote cha maombolezo, wakati maandalizi ya safari ya mwisho ya mmoja wa watu mashuhuri wa kisiasa yakiendelea.

Mazishi yamepangwa kufanyika siku ya Jumapili na yatafanyika kwa mujibu wa mila za  kanisa la African Church ambalo Raila alikuwa muumini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *