Leo ni Ijumaa, tarehe 25 Mehr, 1404 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 24 Rabi’ al-Thani, 1447 Hijiria Qamaria, na inayosadifiana na Oktoba 17, 2025 Miladia.
Miaka 1059 iliyopita, kwa mujibu wa nukuu mbalimbali za kihistoria, mnamo tarehe 24 Rabi’ al-Thani, 388 Hijria, “Abu Ali Muhammad ibn Muzaffar”, aliyejulikana kama Hatami au Baghdadi, mwanafalsafa, mwandishi, na mwanazuoni wa Kiislamu, alifariki dunia. Alisoma sayansi ya fasihi na falsafa na maprofesa wa wakati huo, na baada ya kukusanya maarifa mengi katika uwanja wa fasihi, alianza kufundisha kozi za fasihi huko Baghdad. Kozi ya Hatami ilikuwa tajiri sana kimaudhui, kiasi kwamba Qadi Tanukhi na wanachuoni wengine wakubwa wa wakati huo walihudhuria kozi yake. Miongoni mwa kazi za Hatami, ni kitabu “Hatimia” kinachozungumzia mapungufu ya mashairi na nyimbo za washairi wa kisasa.

@@@@@@@@@@
Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza.
Vikwazo hivyo vilionesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.

@@@@@@@@@@
Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron.
Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vile vile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi.

@@@@@@@@@
Miaka 86 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yani tarehe 25, Mehr mwaka 1318, “Mohammad Farrokhi Yazdi,” mshairi na mwandishi wa habari wa Irani ambaye alipinga udhalimu wa Reza Khan, aliuawa gerezani. Mirza Mohammad Farrokhi Yazdi alizaliwa Yazd mwaka 1267 Hijria. Alifukuzwa shuleni akiwa na umri wa miaka kumi na tano kwa kuandika mashairi muhimu. Alijiunga na kikundi cha kupenda uhuru mwanzoni mwa Mapinduzi ya Katiba. Katika Nowruz 1289 AH, Farrokhi alimkosoa mtawala wa Yazd katika shairi lililoelekezwa kwake, na matokeo yake, kwa amri ya mtawala huyo, midomo yake ilishonwa kwa uzi na sindano na kutupwa gerezani. Mwezi mmoja au miwili baadaye, alikimbilia Tehran na kujiunga na safu ya wapiganaji wa kitaifa. Mnamo mwaka wa 1300 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alichapisha gazeti la Toofan na alikosoa hali hiyo. Alichaguliwa katika Bunge la Kitaifa la Iran katika muhula wa saba na watu wa Yazd na kuendeleza mapambano yake, lakini baadaye, kutokana na ukosefu wa usalama, alikimbilia Moscow na kutoka huko hadi Ujerumani. Farrokhi baadaye alirudi Iran, na kisa baadaye alikamatwa na kufungwa, na aliuawa akiwa na umri wa miaka 51.

@@@@@@@@@@
Na leo tarehe 17 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini Duniani. Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umaskini. Mwaka 1992 Umoja wa Mataifa uliitangaza siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.”
Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa, kila mwanadamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung’oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.
