Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterania limetahadharisha katika taarifa yake kwamba, hatari ya njaa bado haijaondolewa huko Gaza, na kuendelea kupunguzwa kwa makusudi misaada ya kibinadamu kunadhihirisha kuwa utawala wa Israel unaendelea kutumia sera ya njaa kama wenzo wa mauaji ya halaiki.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterania limetangaza katika taarifa yake kuwa: “Kiasi kidogo cha bidhaa na misaada ambayo utawala wa Israel umeruhusu kuingia Gaza kinahudumia sehemu ndogo tu ya mahitaji halisi ya watu.”

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilionyesha wasiwasi zaidi kwamba Tel Aviv inatishia kupunguza misaada ya kibinadamu na kutofungua kivuko cha Rafah kwa kutumia visingizio kama vile kutokabidhi miili ya Waisraeli waliouawa.

Kadhalika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterania, katika siku mbili baada ya kutangazwa usitishaji vita huko Gaza, utawala wa Israel uliruhusu malori 173 pekee yaliyobeba misaada ya kibinadamu kuingia katika Ukanda huo, huku kukiwa hakuna lori lolote lililoingia Gaza siku ya Jumatatu, Oktoba 13, na siku ya Jumanne, misaada pia ilisitishwa kutokana na likizo ya kidini ya Wazayuni.

Shirika hilo pia limesisitiza kuwa: Udhibiti wa utawala wa Israel juu ya wingi wa misaada na kupuuza majukumu yake chini ya makubaliano ya usitishaji vita kuna maana ya kuendelea kutekeleza jinai ya mauaji ya kimbari.

Taarifa hiyo imesisitiza zaidi kwamba, kuingia misaada ya kibinadamu si fursa au neema ya utawala wa Kizayuni, bali ni wajibu wa kisheria usioweza kujadiliwa, na kwamba misaada ya kibinadamu lazima itolewe kwa kuzingatia kanuni ya kutoegemea upande wowote na kwa mahitaji ya binadamu pekee, bila ya ubaguzi, kucheleweshwa au kuchagua.

Wapalestina wakiwa katika safu za msaada wa chakula

Chombo hiki cha kimataifa kimetoa wito wa kusitishwa kikamilifu operesheni za kijeshi na kuondolewa mara moja na kwa kina mzingiro wa Gaza, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa dhamana ya kimataifa ili kuzuia kurudiwa kwa mzingiro huo au kuzuiwa kwa misaada kuingia Ukanda huo kwa kisingizio chochote.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni unatumia visingizo mbalimbali hivi sasa kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa hivi karibuni kati yake na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano wiki iliyopita, kulingana na mpango uliowasilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Awamu ya kwanza ya mpango huo inajumuisha kuachiliwa huru mateka wa Israel mkabala wa kuachiwa huru Wapalestina waliokuwa wakiteseka kwenye magereza ya utawala huo ghasibu.

Siku ya Jumanne, Israel ilitishia kupunguza kwa asilimia 50 kiwango cha misaada ya kibinadamu inayoruhusiwa kupelekwa Gaza, chini ya makubaliano tete ya kusitisha mapigano na Hamas.

Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, ameitaka Israel kufungua mara moja vivuko zaidi katika Ukanda wa Gaza ili kuruhusu ongezeko la utoaji wa misaada.

Hapo awali, Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu zilitoa wito wa kufunguliwa njia zote za vivuko vya kuingilia Gaza ili kuruhusu misaada inayohitajika sana katika ardhi hiyo ya Palestina iliyowekewa mzingiro.

Hapana shaka kuwa, hatua hizi mpya za ukwamishaji zinazofanywa na Israel zinazidi kuthibitisha kwamba, utawala huo ghasibu hauko tayari kuheshimu makubaliano ya aina yoyote unayofikia na upande wa pili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *