
Kiongozi mpya wa kijeshi nchini Madagascar Kanali Michael Randrianirina ataapishwa kuwa Rais mapema leo Ijumaa. Amesema pia kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na Umoja wa Afrika baada ya taasisi hii kuifutia uanachama nchi yake.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kanali Randrianirina ataapishwa kama rais wa Jamhuri ya Madagascar leo Ijumaa katika Ikulu ya rais ya Ambohidahy, makao makuu ya Mahakama Kuu ya Katiba, anaripoti mwandishi wetu huko Antananarivo, Guilhem Fabry. Kiongozi huyo mpya wa Kisiwa hiki kikubwa alitangaza kuvunjwa kwa taasisi hii siku ya Jumanne alasiri baada ya kuchukua mamlaka, kabla ya taasisi hiyo, katika uamuzi uliochapishwa saa moja baadaye, kumtaka kuchukuwa madaraka kama Mkuu wa Nchi.
Katika kauli aliyoitoa juzi Jumatano Kanali Michael Randrianirina amethibitisha kuwa ataapishwa kuushika wadhifa wake mpya kama Rais wa Madagascar. Anatazamiwa kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito cha hadi miaka miwili.
Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo wa kijeshi alikuwa na jukumu muhimu katika kikosi maalumu kilichofanya mapinduzi mwaka 2009 na kumweka madarakani Andry Rajoelina. Hata hivyo katika maandamano ya hivi karibuni kikosi hicho kilimpa kisogo kiongozi huyo na kuamua kuwa upande wa wananchi ambapo kiliwataka polisi wasiwafyatulie risasi waandamanaji.
Maandamano hayo ya kuipinga serikali yake yalianzishwa na vuguvugu lililoongozwa na vuguvugu la vijana maarufu Gen Z Septemba 25 wakilalamikia ukosefu wa maji na huduma za umeme. kiongozi mpya Kanali Randrianirina atakapoapishwa keo atawaongoza takriban watu milioni 30. Robo tatu ya raia hao wanaishi katika dimbwi kubwa la umasikini.
Utawala mpya wa kijeshi unatazamiwa kuapishwa wakati Umoja wa Afrika (AU) ulitangaza juzi kuwa umeifuta Madagascar uanachama kutokana na mapinduzi yaliyomwondoa madarakani Rais Andry Rajoelina.
Umoja huo pia ulitoa wito kwa taifa hilo kurejesha utawala wa kiraia na kufanya uchaguzi.Akizungumzia uamuzi wa chombo hicho Kanali Randrianirina alisema mapema Alhamisi kwamba ni hatua iliyokuwa ikitegemewa na kwamba kuanzia sasa kutakuwa na mazungumzo ya faragha.
Kuondolewa kwa Madagascar katika Umoja wa Afrika kunabeba uzito kisiasa na kunaweza kuutenga utawala mpya. Wakati huohuo kwa mara ya kwanza Rais Andry Rajoelina amethibitisha kuwa aliikimbia nchi baada ya maandamano makubwa ya wiki kadhaa.
Rajoelina aliondoka kati ya Oktoba 11 na 12 baada ya kile ofisi yake ilichokiita kuwa “vitisho vikali dhidi ya maisha ya mkuu wa nchi”.