Marekani. Mrembo na mfanyabiashara maarufu, Kim Kardashian, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu hali ya malezi ya watoto wake na mwanamuziki Kanye West, ambaye pia ni mume wake wa zamani.

Akiwa mgeni katika kipindi cha podcast Call Her Daddy kilichoendeshwa na Alex Cooper Jumatano, Oktoba 15, Kim alizungumzia mambo mengi kuanzia maisha yake ya kimapenzi hadi changamoto za kulea watoto wanne na Kanye, ambaye amekuwa akigonga vichwa vya habari mara kwa mara kutokana na tabia na matamshi yake tata.

“Unadhani kulea watoto na Kanye West ni kama nini?” Kim alimchekesha mtangazaji kwa kuuliza kabla ya kujibu mwenyewe.

KARDA 04

“Sio rahisi,” alikiri mwanzilishi wa SKIMS. “Nawalea watoto muda wote. Wanaishi nami. Ninakaribisha uhusiano mzuri na wenye afya kati ya watoto na baba yao, na naamini anajua hilo.”

Kim ameongeza kuwa amekuwa akijitahidi kuweka uhusiano huo katika hali nzuri lakini pia anawalinda watoto wake inapobidi.

“Mara nyingine mambo yanakuwa mazuri, kisha yanabadilika. Ni kazi kubwa sana,” amesema.

Akimlinganisha Kanye kama baba na marehemu baba yake, Robert Kardashian Sr., Kim amesema angependa watoto wake wawe na ukaribu kama aliokuwa nao na baba yake. Pia alitaja mfano wa dada yake Khloe Kardashian, ambaye anashirikiana vyema kulea mtoto wake na mchezaji wa mpira wa kikapu Tristan Thompson.

KARDA 01

“Ninaona jinsi Tristan anavyoweka bidii analala na watoto wake kila usiku na kuwapeleka shule kila siku anapokuwa nyumbani. Ningeweza kuona kitu kama hicho kwetu pia, lakini sio rahisi,” aliongeza Kim.

Alipoulizwa ni lini mara ya mwisho Kanye aliwasiliana na watoto, Kim amesema:

“Ni pale tu anapowapigia simu. Kwa sasa, imepita kama miezi michache tangu tusikie kutoka kwake.”

Watoto wa wanandoa hao wa zamani ni North mwenye umri wa miaka 12, Saint (miaka 9), Chicago (miaka 7) na Psalm (miaka 6).

Kim alieleza kuwa watoto wake wanaelewa maisha ya baba yao ambayo mara nyingi yanahusisha safari na kazi nyingi.

KARDA 03

“Wanajua kuwa alikuwa akisafiri sana kwa kazi, hivyo tumekuwa tukisimamia hali hiyo vizuri. Wanapenda maisha yao na ratiba zao. Kazi yangu kama mama ni kuhakikisha wanabaki kwenye utaratibu wao, afya njema na furaha,” amesema.

Akiweka bayana upande wake kuhusu tuhuma za Kanye kwamba anamnyima watoto, Kim amesema: “Kuna simulizi ambalo haliko sahihi kwamba ninawazuia watoto. Sijawahi kufanya hivyo hata mara moja. Wakati mwingine natamani nionyeshe meseji zote ninazomtumia nilikuwa namsihi aje kuwaona watoto.”

KARDA 02

Kim alimalizia kwa kueleza matumaini yake kuwa siku moja wataweza kuwa na uhusiano wa kifamilia uliokomaa zaidi.

“Ningependa tuwe tunaweza kula chakula pamoja kama familia. Nililelewa nikiona wazazi wangu wakishirikiana vizuri. Ninaliona hilo kwa Khloe na Tristan pia uhusiano wenye afya ni kitu kizuri,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *