Jeshi la Nigeria limetoa taarifa na kutangaza kuwa makumi ya waasi wameuawa na wengine 62 kukamatwa na vikosi vya serikali katika operesheni za nchi nzima kwenye kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria, msemaji wa jeshi la nchi hiyo, Markus Kangye amesema kuwa, majeshi ya Nigeria yamefanikiwa pia kukomboa watu 30 waliokuwa wametekwa nyara na magenge ya kigaidi na kihalifu.

Amesema kuwa, katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria, wanajeshi, kupitia operesheni kabambe ya ardhini na angani, wamepata “mafanikio makubwa” katika majimbo ya Adamawa, Borno na Yobe, ambapo kwa uchache washirika 16 na majasusi wa vikundi vya waasi wamekamatwa. Takriban mateka saba wamekombolewa katika eneo hilo pekee, pamoja na silaha na risasi mbali na kuharibiwa maficho ya wahalifu hao.

Katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Nigeria, vikosi vya serikali vimezima mashambulizi na kuua au kuwakamata washukiwa wa uhalifu wakati wanajeshi walipokuwa wanaimarisha doria.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria pia amesema: Katika kipindi hicho cha wiki mbili, kamanda maarufu wa genge lililopigwa marufu la  Watu wa Asilia wa Biafra na tawi lake la kijeshi wamekamatwa pamoja na vifaa vyao wakiwemo pia mamluki wa genge hilo waliokuwa wamejificha kwenye jamii kwa kazi mbalimbali kama wauzaji wa bidhaa za kike.

Vilevile Kangye amesema: “Vikosi vya Kijeshi vya Nigeria vitaendelea na mapambano yake ya kutokomeza ugaidi, ujambazi na vitisho vingine vya usalama kote nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *