Dar es Salaam. Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), kupitia mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati ya Tanzania, umekabidhi rasmi kifaa cha kupima hewa isiyo safi kwenye majiko kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuimarisha juhudi za Upimaji wa Majiko yanayotumika Kupikia nchini.

Makabidhiano haya ni sehemu ya Utekelezaji wa Mradi wa CookFund unaolenga kuharakisha usambazaji wa nishati safi ya kupikia Tanzania.

Mashine hii itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwezo wa TBS kupima na kuchambua kwa usahihi moshi mchafu unaotoka kwenye teknolojia za kupikia safi, iwe ni zimetengenezwa nchini au zilizoagizwa kutoka nje.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio; “Hii ni hatua kubwa katika kuendeleza harakati za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Nina furaha kushiriki tukio hili muhimu la makabidhiano kwani kifaa hiki kitatumika maalum kabisa kupima aina ya gesi au moshi mchafu unaotokana na matumizi ya majiko yanayotengenzwa au kuingizwa hapa nchini.

TBS sasa itaweza kuthibitisha ubora wa vifaa vya kupikia safi, kupunguza gharama za upimaji, na kusaidia wabunifu kuongeza uzalishaji.”

Serikali ya Tanzania imekuwa ikihamasisha ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na mkakati wa mawasiliano, ambazo zote zinalenga kuhakikisha asilimia 80 ya kaya zinazotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Umoja wa Ulaya unajivunia kuwa sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania. Tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi kama tunavyofanya kupitia Mradi wa CookFund na programu nyingine zinazofanana na hizo. Tunatarajia kifaa hiki kitawanufaisha zaidi wabunifu na wazalishaji—hasa kwa kupunguza gharama za upimaji.

Hii itachochea ubunifu na kuongeza kazi ya utengenezaji majiko na kuharakisha upimaji na usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi” alisema Marc Stalsmans, Mkuu wa Ushirikiano, EU Tanzania

Mradi wa CookFund, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na UNCDF kwa niaba ya Wizara ya Nishati, umetoa ruzuku kwa wafanyabiashara wa kati (SMEs) na kuboresha uwezo wa mashirika mbalimbali kama njia ya kusaidia usambazaji wa teknolojia za kupikia safi sokoni.

Mradi huu hadi sasa umetoa ruzuku kwa biashara 78, kusaidia shule 41 kuanza matumizi ya Nishati safi ya kupikia, kunufaisha zaidi ya watu milioni 1.7, kutengeneza zaidi ya ajira 11,600 na sasa unasaidia utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya matumizi ya Nishati safi ya Kupikia nchini Tanzania. 

“UNCDF, tunaamini kuwa kifaa hiki cha kupima hewa kiwango cha hewa chafu kitatoa takwimu muhimu za kutathmini athari halisi za majiko ambayo hayajakidhi viwango ambayo yanaweza kuwa na athari kwa watumiaji na kuharibu mazingira.

Tunajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania, EU, na washirika wengine wa maendeleo ili kufanya upishi safi kuwa halisi kwa Watanzania wengi,” alisema Bwana Shigeki Komatsubara, Mwakilishi wa UNCDF Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura A. Katunzi, aliipongeza Serikali na Washirika kwa kuiwezesha TBS kuongeza uwezo wa kupima na kusanifisha majiko.

“Kupatikana kwa kifaa cha upimaji hapa TBS Dar es Salaam ni hatua muhimu katika kupunguza gharama za upimaji, jambo litakalotusaidia kusogea karibu zaidi na usanifishaji wa vifaa vya kupikia safi nchini Tanzania. Tunaomba msaada zaidi ili tuweze kupanua huduma hizi hadi kwenye vituo vyetu vilivyopo kwenye mikoa mingine kama Dodoma, Mbeya na Mwanza”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *