Video ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP nchini Zambia inamuonesha Judith Mabeta mama wa watoto sita na wajukuu watatu akitoka kwenye nyumba yake iliyoezekwa na bati na kwenda jikoni

Judith anasema Nilijiunga na kikundi cha kuweka akiba mwaka 2021, hapo awali nilikuwa nikilala kwenye nyumba iliyokuwa ikivuja, nikaja na wazo la kujenga nyumba. Kutoka kwenye fedha tulizokuwa tukiwekeza kwenye kikundi nikanunua miti na kujenga nyumba, baadae nikanunua mabati na kuezeka, na sasa mimi na familia yangu tumehamia kwenye nyumba kubwa na ninaushukuru mradi wa SCRALA kwakutufundisha kuweka akiba kwani kumetusaidia sana.”

SCRALA ni mradi unaowejengea uwezo wanawake na vijana hususani wakulima na kuwafundisha kuwa na mali kama vile nyumba ili kuboresha maisha yao.

Mradi huu unaendeshwa na Wizara ya Kilimo nchini Zambia chini ya ufadhili wa Mfuko wa kijamii unaojali mazingira GCF na msaada wa kiufundi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo UNDP.

Utekelezaji wa mradi huu ni hatua moja wapo ya kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs hususan lengo namba moja la kutokomeza umasikini.

Ripoti ya UNDP kuhusu umasikini iliyotolewa hii leo imeonesha kuwa watu milioni 887 duniani wanaishi katika umaskini wakizungukwa na hatari za mabadiliko ya tabianchi kama vile joto kali, mafuriko, ukame, au uchafuzi wa hewa. Unaweza kusoma zaidi kuhusu ripoti hii ya katika wavuti wetu wa www.news.un.org/sw

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *