Watu wasiopungua 33 wamefariki dunia kutokana na homa ya Bonde la Ufa nchini Senegal na Mauritania tangu kuzuka kwa mripuko wa homa hiyo nadra mwishoni mwa Septemba, afisa wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) alisema hayo jana Alkhamisi.

Takwimu zilizotolewa na Yap Boum II, Naibu Mkurugenzi wa Matukio katika Afrika CDC, zilionyesha ugonjwa huo umeua watu wasiopungua 20 nchini Senegal, huku kiwango cha vifo katika mikoa mitano ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi ikiwa 11.7%.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu masuala muhimu ya afya katika bara zima, Yap alisema kesi 171 zilizothibitishwa za homa hiyo zimerekodiwa.

Eneo la kaskazini la Saint-Louis ndilo lililoathiriwa zaidi, likinakili kesi 159 kati ya visa vyote vilivyorekodiwa tangu kuthibitishwa kesi ya kwanza wa homa ya RVF nchini humo Septemba 20.

Takwimu hizo pia zilionyesha kuwa nchini Mauritania, homa ya Bonde la Ufa imeua watu 13, huku kesi 36 zikirekodiwa. Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa unaoenezwa na mbu ambao huathiri mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo. 

Wanadamu wanaweza kuambukizwa kupitia kung’atwa na mbu au kugusana na wanyama walioambukizwa, hasa wakati wa kuchinja.

Maambukizi makali ya homa ya Bonde la Ufa yanaweza kusababisha  kuvimba kwa ubongo, kupofuka macho au homa ya kuvuja damu, hali ambazo zinaweza kusababisha kifo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa wafugaji, wakulima, na wafanyakazi wa machinjio ya mifugo wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa homa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *