Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Winnie Odinga, ameelezea namna kifo cha baba yake, marehemu Raila Odinga kilivyotokea akibainisha kuwa hakikuwa kama kinavyoelezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, katika shughuli ya kitaifa ya kuaga mwili wa marehemu Raila Odinga inayofanyika katika Uwanja wa Nyayo, Winnie amesema alikuwa nchini India wakati baba yake alipovuta pumzi yake ya mwisho.

“Nilikuwa India wakati alipofariki. Alifia mikononi mwangu, lakini hakufa kama watu wanavyoeleza kwenye mitandao ya kijamii. Baba alikuwa na afya njema,” amesema na kuongeza kuwa:

“Alikuwa akiamka kila siku kufanya mazoezi ya kutembea siku ya kwanza raundi moja, siku ya pili raundi mbili, siku ya tatu tano na aliendelea hivyo. Naweza kusema baba amefariki akiwa mtu mwenye nguvu na afya njema. Mfalme amelala, lakini urithi wake utaishi milele,” amesema Winnie.

Katika hatua nyingine, Winnie amemtaja baba yake kama kiongozi wa kweli, mwenye upendo na heshima kwa familia, hasa wajukuu zake.

“Alikuwa baba aliyejitoa kwa familia. Hata akiwa ametingwa na majukumu ya kitaifa, hakusahau wajukuu zake; alituma ujumbe wa upendo kila mara,” amesema.

Aidha, amemtaja Odinga kama “baba na shujaa” ambaye hekima, ujasiri na upendo wake vilibadilisha maisha yake.

“Sijui nitamkosa nani zaidi, baba yangu au shujaa wangu, mimi ndiye msichana mwenye bahati kwa sababu ulikuwa baba yangu. Ni watu watatu tu waliokuwa na bahati kama mimi, Fidel, Rozzy na Junior, amesema Winnie.

Amesema Odinga alikuwa mwanga usiobadilika na binadamu ambaye alihamasisha kila mtu aliyekutana naye.

“Kwa ulimwengu, ulikuwa na majina mengi, na uliwapa watu majina ya utani kila mara. Lakini kwangu, ulikuwa tu Baba,” amesema.

Akimkumbuka nyumbani kwao, Winnie amesema baba yao alikuwa akiwachochea kufikiri zaidi kupitia maswali na vitendawili.

“Nyumba yetu ilikuwa kama uwanja wa majaribio ya vitendawili. Baba alipenda kutupa changamoto za kufikiri, na zilituimarisha sana,” amesema.

Aidha, amegusia ombi la mwisho la baba yake kuwa azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake, akisema alicheka kwa upole aliposikia hilo, akieleza kuwa lilikuwa sawa kabisa na hulka ya baba yake kwani alikuwa mtu wa uamuzi, uthabiti na anayependa maisha yenye maana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *