
Rais wa Russia, Vladimir Putin amemuonya Rais wa Marekani, Donald Trump katika mazungumzo yao ya simu kwamba, kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu ya Tomahawk kutaharibu zaidi uhusiano kati ya Moscow na Washington.
Katika mazungumzo ya karibu saa mbili na nusu jana Alkhamisi, Putin alisisitiza kwamba ingawaje makombora haya hayatabadilisha hali katika medani ya vita, lakini yanaweza kuharibu kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kidiplomasia na kuzuia juhudi za amani nchini Ukraine, hayo ni kwa mujibu wa msaidizi wa Rais wa Russia, Yuri Ushakov.
Wakati wa mazugumzo hayo, Putin amemfahamisha Trump kwamba Russia inashikilia “mpango kamili wa kimkakati” katika mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.
Trump, kwa upande wake, amesisitiza kuwa kumaliza mzozo huo kutaleta fursa kubwa za ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Baada ya mazungumzo hayo, Trump alitangaza kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba yeye na Putin wanapanga kukutana nchini Hungary ili kujadili zaidi mzozo unaoendelea, baada ya wajumbe wa ngazi ya juu kukutana wiki ijayo.
Kabla ya hapo, Putin alisema ikiwa Marekani itaipatia Ukraine makombora aina ya Tomahawk ili kufanyia mashambulio ya masafa marefu ndani ya Russia, hatua hiyo itapelekea kuvurugika husiano wa Moscow na Washington.
Jeshi la Russia limesema linachunguza iwapo Marekani itaikabidhi Ukraine makombora ya meli ya Tomahawk au la kwa ajili ya kutekeleza mashambulizi dhidi yake; na kuonya kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha mzozo mkubwa.