Rais wa Madagascar aliyeondolewa madarakani Andry Rajoelina amethibitisha kwa mara ya kwanza kwamba aliikimbia nchi hiyo kati ya Oktoba 11 na 12.

Rajoelina amesema aliikimbia nchi hiyo ya kisiwa kufuatia kile alichotaja kuwa vitisho vya wazi kwa uhai wake.

Jeshi ambalo lilitangaza kunyakua madaraka limetangaza kuwa kiongozi wao Kanali Michael Randrianirina ataapishwa rasmi leo Ijumaa kuwa rais mpya wa Madagascar.

Kanali Michael Randrianirina ametakiwa na Mahakama ya Katiba kuitisha  uchaguzi ndani ya siku 60 kwa mujibu wa siku atakayoamua, ikinukuu Kifungu cha 53 cha Katiba, ambacho kinahitaji uchaguzi wa urais ufanyike ndani ya siku 30 hadi 60 baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kutangaza kuwa ofisi hiyo imebaki tupu.

Jumuiya ya kimataifa inapinga hatua hiyo na imewataka wadau wote wa Madagascar kutafuta suluhisho la amani linaloheshimu katiba ya nchi hiyo.

Umoja wa Afrika umetengaza kuisimamishia unachama Madagascar “hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa” baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Andry Rajoelina.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema, utawawekea watu makhsusi vikwazo iwapo utawala wa kiraia hautarejeshwa nchini humo. Huko nyuma pia, jumuiya hiyo ilisimamishia nchi kadhaa uanachama baada ya mapinduzi ya kijeshi, zikiwemo Mali, Burkina Faso na Guinea.

Tangu Septemba 25, Rajoelina amekabiliwa na maandamano yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen-Z wanaolalamikia uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa; maandamano ambayo yameenea haraka kote nchini na kugeuka kuwa mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *