Hayo yamebainishwa katika ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo duniani (UNDP) kwa ushirikiano na Taasisi ya Masuala ya Umaskini na Maendeleo ya Binadamu ya Chuo Kikuu cha Oxford (OPHI), ya mwaka 2025 ya Kiashiria cha MPI, yenye kichwa “Changamoto Zinazoshirikiana: Umaskini na Hatari za Tabianchi”, ambayo kwa mara ya kwanza imeonesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya umaskini na majanga ya kimazingira, huku ikitolewa mwezi mmoja kabla ya Mkutano wa COP30 nchini Brazil.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wanaoishi katika umaskini katika nyanja nyingi—ambao hupimwa kupitia vigezo vya afya, elimu na viwango vya maisha—wanakabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati mmoja.

Utafiti wetu umeonesha kuwa ili kupambana na umaskini duniani na kuhakikisha ustawi wa kudumu, ni lazima tuchukue hatua dhidi ya hatari za mabadiliko ya tabianchi zinazowaathiri vibaya  karibu watu milioni 900 maskini,” amesema Haoliang Xu, Kaimu Mkurugenzi wa UNDP.

Viongozi wa dunia wanapokutana kwenye mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP30, ahadi zao za kitaifa kuhusu tabianchi zinapaswa kuimarisha kasi ya maendeleo na kuhakikisha maskini hawaachwi nyuma,” ameongeza.

Mzigo wa umaskini na hatari za mabadiliko ya tabianchi

Ripoti imeonesha kuwa watu maskini duniani hukabili changamoto nyingi za kimazingira kwa wakati mmoja badala ya moja pekee.

  • Kati ya idadi ya watu milioni 887 wanaoishi katika maeneo yenye hatari za tabianchi, milioni 651 wanakabiliwa na hatari mbili au zaidi.
  • Watu milioni 309 wanakabiliwa na hatari tatu au nne za mazingira wakiwa katika umaskini mkali wa vipengele vingi (MPI).
  • Hatari kuu zaidi ni joto kali (watu milioni 608) na uchafuzi wa hewa (milioni 577), huku maeneo yenye mafuriko yakihifadhi watu milioni 465, na ukame ukiathiri milioni 207.

Ripoti hii inaonesha wazi maeneo ambayo umaskini na mabadiliko ya tabianchi vinakutana kwa nguvu zaidi,” amesema Sabina Alkire, Mkurugenzi wa OPHI. “Kuelewa maeneo ambako binadamu na mazingira vinapata shinikizo kubwa ni hatua muhimu kuelekea sera za maendeleo zinazounganisha ustawi wa watu na hatua za kulinda sayari,” ameongeza

Je ni yapi maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi ?

Mzigo wa changamoto hizi unaonekana zaidi katika maeneo ya Asia Kusini na nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

  • Asia Kusini ina idadi ya watu milioni 380 wanaoishi katika maeneo yenye hatari za tabianchi—sawa na asilimia 99.1 ya maskini wote wa eneo hilo.
  • Katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, watu milioni 344 wanaishi katika mazingira kama hayo.
  • Nchi zenye kipato cha kati cha chini ndizo zinazoathirika zaidi, zikiwa na idadi ya watu milioni 548 wanaoishi katika umaskini na kukabiliwa na zaidi ya hatari moja ya mabadiliko ya tabianchi, huku milioni 470 wakiwa na zaidi ya changamoto mbili kwa wakati mmoja.

Ni nini mustakabali wa hali hii?

Mzigo huu wa changamoto sio wa sasa pekee, bali unatarajiwa kuongezeka zaidi katika siku zijazo,” amesema Pedro Conceição, Mkurugenzi wa Ofisi ya Ripoti za Maendeleo ya Binadamu wa UNDP. “Takwimu za makadirio ya joto zimeonesha kuwa nchi zenye viwango vya juu vya umaskini wa vipengele vingi (MPI) kwa sasa ndizo zitakazopata ongezeko kubwa zaidi la joto kufikia mwisho wa karne hii.”

Ripoti imetoa wito wa hatua za haraka za kimataifa, zikiwemo mikakati ya kupunguza umaskini inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uwezo wa jamii kujihami, na ushirikiano wa kifedha kusaidia mataifa yaliyo hatarini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *