Mbeya. Zaidi ya Sh228 milioni zimetumika kuboresha miundombinu ya jengo na vifaa muhimu katika wodi ya watoto wachanga ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, ikiwa ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa njiti au wenye changamoto za kiafya.

Miongoni mwa maboresho hayo ni ujenzi wa chumba maalumu cha hatamizi kwa wanaume, kitakachowasaidia wazazi wa kiume kushiriki katika huduma za malezi ya awali kwa watoto wao, hususan pale wenza wao wanapopata matatizo ya kiafya baada ya kujifungua.

Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, wakati wa uzinduzi wa wodi hiyo (Neonatal Care Unit NCU), Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya Ifakara (Ifakara Health Institute – IHI), Dk Honorath Masanja amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Nest 360 Tanzania, unaolenga kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini.

“Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya IHI, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wadau wengine, wakiwemo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2019 hadi 2023 ukiwa katika awamu ya kwanza, ukijumuisha hospitali saba nchini,” amesema Dk Masanja.

Amefafanua kuwa lengo la mpango huo ni kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 12 kwa kila vizazi hai 1,000 kufikia mwaka 2030, kwa kuboresha huduma za kitaalamu, miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba.

Dk Masanja ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu, mifumo ya takwimu na vifaa tiba, sambamba na kuhakikisha watoa huduma wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara.

“Kuokoa maisha ya watoto wachanga kunahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu, maarifa na teknolojia. Taasisi yetu itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma bora zinapatikana hadi ngazi ya wilaya,” ameongeza.

Muonekano wa wodi  ya watoto wachanga Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kitengo cha wazazi Meta baada ya kufanyiwa boreshwa kupitia mradi wa Nest 360 Tanzania. Picha na Hawa Mathias

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameipongeza Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wadau wote walioshiriki kuboresha miundombinu hiyo, akisema hatua hiyo ni chachu ya kupunguza vifo vya watoto wachanga.

“Nimetembelea wodi hii na kwa kweli nimeshtuka kuona ukubwa wa changamoto tulizonazo. Nimeguswa na nitaanza kuchangia kitanda kimoja cha watoto wachanga kila mwaka. Naomba wadau wengine waunge mkono juhudi hizi ili kuokoa kizazi chetu cha sasa na kijacho,” amesema Malisa.

Malisa ameongeza kuwa vifo vya watoto wachanga bado ni changamoto kubwa nchini, akibainisha kuwa takribani watoto 50,000 hupoteza maisha kila mwaka, sawa na mtoto mmoja kila baada ya dakika 10.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikifanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo hilo kwa kutoa zaidi ya dola milioni 18 kwa ajili ya ukarabati wa vitengo vya watoto wachanga na ununuzi wa vifaa tiba muhimu katika hospitali za mikoa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa uwekezaji katika rasilimali watu na vifaa vya kisasa, ili kuhakikisha watoto wachanga wanapata huduma bora za kiafya.

“Watoto wachanga wanahitaji uangalizi wa hali ya juu. Watoa huduma wetu wanafanya kazi usiku na mchana bila kuchoka. Tunapaswa kuwapongeza na kuwasaidia. Hata hivyo, bado tunahitaji wadau zaidi kuwekeza katika eneo hili,” amesema Dk Mbwanji.

Ameongeza kuwa pamoja na maboresho yaliyofanyika, hospitali hiyo imeanzisha chumba maalumu cha wanaume ili wanaume waweze kushiriki moja kwa moja katika huduma za hatamizi kwa watoto wao pale wenza wao wanapokuwa hospitalini.

“Tumetenga chumba kwa ajili ya wanaume kusaidia watoto wao wakati wenza wao wanapopata matatizo ya kiafya baada ya kujifungua. Hii ni hatua ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi wa kiume katika malezi tangu hatua za awali,” amesema Dk Mbwanji.

Mkurugenzi mtendaji  Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,Dk Godlove Mbwanji  akizungumza  na wananchi  na watumishi  walioshiriki uzinduzi  wa wodi  ya watoto wachanga katika kitengo cha wazazi Meta. Picha na Hawa Mathias

Katika hali ya ucheshi, alitangaza kuwa kutakuwa na zawadi maalum kwa mwanaume wa kwanza atakayejitolea kutoa huduma ya hatamizi kwa mtoto mchanga, ili kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi.

Kwa upande wake, Janeth Thom, mama aliyejifungua hivi karibuni katika hospitali hiyo, alisifu Serikali na wauguzi kwa huduma bora zinazotolewa, lakini akaomba kupunguzwa kwa gharama za upasuaji wakati wa kujifungua.

“Huduma za afya ya uzazi zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma, lakini bado changamoto kubwa ni gharama kubwa za kujifungua kwa upasuaji. Tunaomba Serikali iangalie jambo hili,” amesema Thom.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *