Dar es Salaam. Msanii na mfanyabiashara maarufu Tanzania, Zuwena Mohammed aka Shilole au Shishi Baby, amewataka mastaa wenzake kupunguza kuagiza raundi wanapokuwa kwenye starehe za unywaji pombe badala yake siku moja moja wajitoe kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima.

Akipiga stori na Mwananchi, Shilole aliwataka wasanii kuiga mfano wa watu ambao hujitoa kwa watoto yatima kwani kwa kufanya hivyo mambo yao mengi yatafunguka.

“Jamani mie nashauri kitu kimoja, tupunguze raundi za kuagiza pombe tunapokuwa kwenye starehe wasanii wenzangu, badala yake tujitoe sana kwa watoto yatima, ili mambo yetu yatuendee, ujue hata hawa watu wenye kipato kikubwa, siyo kwamba walilala na kuamka matajiri, wao wamekuwa wakijitoa sana kwenye jamii isiyojiweza,” amesema Shilole.

Shilole amekuwa ni mmoja wa wasanii wenye kutoa msaada mara nyingi kwenye vituo vya watoto yatima na hata inapofika mwezi wa Ramadhani hupenda kufuturisha watoto yatima.

Mbali na hayo, Shilole amewashauri vijana wa kike na kiume kutumia vizuri vipaji vyao ili kuishi maisha ya ndoto zao.

Amesema yeye ni mmoja wa watu waliotumia vipaji vizuri na maisha yamemnyookea tofauti na msoto aliopitia wakati anajitafuta.

“Umaarufu nilionao hivi sasa umetokana na kuthamini kipaji nilichonacho na kukifanyia kazi, leo namshukuru Mungu maisha yangu ni mazuri namiliki nyumba, usafiri na familia yangu haina shida ndogondogo,” amesema Shilole.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *