Wakati janga la afya duni ya macho likiwanyemelea Watanzania wengi, wataalamu wa afya wamesisitiza umuhimu wa lishe bora katika kuboresha afya ya macho, wakieleza kuwa vyakula vya asili kama mboga za majani na matunda yenye rangi ya machungwa vina mchango mkubwa katika kujenga kinga ya mwili na kuimarisha uwezo wa kuona, hasa kutokana na uwepo wa kirutubisho muhimu cha Vitamin A.

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, David Gambo, anasema Vitamin A ni kirutubisho cha lazima kinachohitajika kwa kiasi kidogo lakini chenye athari kubwa kwa afya ya macho, ukuaji wa watoto, na uimara wa kinga ya mwili.

“Vitamin A husaidia macho kuona vizuri hasa nyakati za usiku, huimarisha kinga ya mwili na kuchochea ukuaji wa seli za ngozi na tishu za ndani ya mwili,” anasema Dk Gambo.

Anaongeza kuwa uhaba wa Vitamin A mwilini unaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya macho ikiwemo upofu wa usiku, ukavu wa macho  na kupungua kwa uwezo wa mwili kupambana na magonjwa, hasa kwa watoto na wajawazito.

Kwa mujibu wa Dk Gambo, Vitamin A hupatikana katika makundi mawili ya vyakula: vya asili ya wanyama na vya asili ya mimea.

 “Vyakula vya wanyama kama ini, mayai na samaki wenye mafuta vimejaa Vitamin A kamili. Vyakula vya mimea kama mboga za majani na matunda ya rangi ya machungwa vina beta-carotene, ambayo hubadilishwa na mwili kuwa Vitamin A,” anaeleza.

Mboga za kijani kibichi kama mchicha, sukuma wiki, kisamvu, spinachi na majani ya maboga ni miongoni mwa vyakula tajiri kwa beta-carotene. 

Hata hivyo, Dk Gambo anasisitiza umuhimu wa kuzipika kwa uangalifu ili zisipoteze virutubisho vyake.

Anashauri mboga hizo zichomwe kwa muda mfupi (dakika 3–5) katika maji yaliyochemka au kupikwa kwa mvuke. Aidha, kuongeza mafuta kidogo kama ya alizeti au mawese husaidia mwili kufyonza Vitamin A vizuri zaidi kwa kuwa ni ya mumunyifu kwenye mafuta.

 “Watu wengi hupika mboga kwa muda mrefu na kwa moto mkali, jambo linalosababisha kupotea kwa Vitamin A. Ni vyema kutumia moto wa wastani na maji kidogo,” anasisitiza.

Matunda ya rangi ya machungwa

Matunda kama karoti, papai na maembe yaliyoiva pia yanatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha carotene. 

Dk Gambo anashauri matunda haya yatumike mara kwa mara, hasa kwa watoto na wanawake wajawazito, kwani huchangia kuimarisha kinga ya mwili na ukuaji wa mtoto.

 “Karoti unaweza kuchemsha dakika chache tu na kuongeza mafuta au parachichi ili kuongeza ufanisi wa ufyonzaji wa carotene,” anashauri.

Upungufu wa Vitamin A, unaojulikana kitaalamu kama Vitamin A Deficiency, bado ni changamoto kwa jamii nyingi Afrika, ikiwemo Tanzania. Dk Gambo anasema hali hii huathiri zaidi watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito.

Dalili za awali za upungufu huo ni pamoja na macho kuwa makavu, kuona vibaya wakati wa jioni au usiku, macho kuwasha au kutoa uchafu, na watoto kukosa hamu ya kula na kuugua mara kwa mara.

“Watu wengi hawajui kuwa matatizo ya kuona usiku au uchovu wa macho ni ishara ya upungufu wa Vitamin A. Mara nyingi hali hii hupuuzwa hadi inapoathiri uwezo wa kuona,” anasema.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), upungufu mkali wa Vitamin A unaweza kusababisha upofu wa kudumu kwa watoto ikiwa hautatibiwa mapema.

Dk Gambo anatoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha familia zao zinapata lishe yenye mchanganyiko wa vyakula vyenye rangi mbalimbali, hasa vya kijani na machungwa.

“Lishe bora si lazima iwe ghali. Mboga kama mchicha, majani ya maboga au matunda kama papai yanapatikana kwa bei nafuu. Jambo la msingi ni kujua namna bora ya kuandaa,” anasema.

Anahitimisha kwa kusisitiza kuwa afya njema huanzia jikoni, akiwashauri wazazi kuanza kuwafundisha watoto tabia ya kula mboga na matunda kila siku.

 “Kila mlo unaoliwa nyumbani ni nafasi ya kujenga au kuharibu afya. Tujifunze kupika kwa uangalifu na kulinda afya zetu kupitia lishe sahihi,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *