
Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta, amesema kuwa marehemu Raila Amolo Odinga alikuwa “Baba wa Taifa” kutokana na mapenzi yake makubwa kwa Kenya na kujitolea kwake katika kulinda misingi ya haki, umoja na demokrasia.
Akizungumza leo Ijuma, Oktoba 17, 2025 wakati wa shughuli ya kitaifa ya kuaga mwili wa Raila iliyofanyika katika Uwanja wa Nyayo, Uhuru amesema kuwa Wakenya walimfahamu Odinga kwa majina mengi ya utani kama Jakom, Agwambo, na Ting’a, lakini zaidi ya yote, walimjua kama Baba.
“Tuko hapa leo kama Wakenya kusherehekea maisha ya kiongozi mwenzetu, rafiki yangu na ndugu yangu. Mheshimiwa Raila Amolo Odinga tulimjua kwa majina tofauti tofauti-Jakom, Agwambo, Ting’a- lakini kama taifa tulimjua na tukamheshimu kama Baba,” amesema Uhuru.
Ameeleza kuwa Raila alipendwa kwa sababu ya maono yake, fikra zake, na matendo yake, si kwa sababu ya kabila au rangi yake.
“Mheshimiwa Raila alipenda nchi yake kuliko kitu kingine chochote. Hakuwa na ukabila. Alipenda Kenya yote na wananchi wake wote. Nyumbani kwake ulikutana na marafiki kutoka kila kona ya taifa letu – hilo lilikuwa somo la umoja na upendo wa kweli,” amesema.
Uhuru amesisitiza kuwa historia ya Kenya haiwezi kuandikwa bila jina la Raila Odinga.
“Historia ya demokrasia ya Kenya haiwezi kuandikwa bila jina la Raila Odinga likiwa namba moja. Historia ya haki za binadamu na haki za wananchi haiwezi kuandikwa bila jina lake. Hata historia ya ugatuzi na nguvu za wananchi mashinani haiwezi kutajwa bila kumtaja Raila Amolo Odinga,” amesema.
Akimkumbuka kwa uchungu na heshima, Rais Mstaafu Kenyatta alisema Raila ameondoka kimwili lakini ataendelea kuishi katika roho na nafsi za Wakenya wote.
“Raila alipenda amani. Alipenda umoja wa taifa letu. Alipenda kuona Wakenya wakishirikiana kujenga nchi yao pamoja. Alikuwa mteule wa haki za watu wote, na alipokuwa anaona hakuna haki, alikuwa wa kwanza kusimama kuhakikisha haki inapatikana,” amesema.
Uhuru amehitimisha hotuba yake kwa wito wa kizalendo kwa Wakenya wote kutetea misingi aliyoiamini Raila Odinga.
“Tunapomuaga leo, tuape kama Wakenya kwamba hatutaruhusu haki za binadamu, demokrasia na maadili aliyoyasimamia Raila yarudi nyuma. Tutasonga mbele tukizingatia yale aliyotupigania sisi tulio hai na wale watakaokuja baada yetu. Hivyo ndivyo tutakavyoheshimu alama ya mchango wake kama kiongozi wetu.” amesema.