
Video inaanzia kaunti ya Busia, nyumba ya udongo yenye paa la bati imetwama kiasi kwenye maji, lakini ndio kimbilio la Beatrice Nabwire Okumu. Yeye ni mama na akiwa na mwanae ndani ya nyumba hii anasimulia huku nyumba yake iliyoko jirani paa lake limetwama kabisa ndani ya maji.
“Nilikuja hapa kwa sababu ya mafuriko, niliathiriwa kwangu ndio maana nilikimbilia kwa Jirani. Maji yaliingia ndani ya nyumba na kulibeba. Huyu mtoto wangu mmoja ambaye nimembeba, alikuwa hatarini nikamweleza Mhamasishaji wa Afya ya Jamii. Madaktari walipokuja wakampima na wakaona yuko hali mbaya wakampa unga vyenye virutubisho aina ya plumpy nuts (Ready-to-Use) ili nimwekee kwa uji na nimpe alambe. Afya yake ilichunguzwa kwa hiyo wiki ya pili nikaona amekuwa sawa.”
UNICEF inasema kuwa jamii zilizohamishwa na mafuriko Magharibi mwa Kenya zinapitia changamoto mbalimbali. Francis Wambua, Mtaalamu wa lishe, UNICEF Kenya anasema,
“Changamoto hizi zinajumuisha ukosefu wa chakula, ukosefu wa makazi bora na kutokuwa na mazingira safi na salama. Na kwa hivyo, mpango huu tumeianzisha, ulikuwa hasa kwa ajili ya kusaidia jamii hizi ziweze kuendelea na maisha ya kawaida licha ya changamoto hizo.”
Electrine Nabwire, Mhamasishaji wa Afya ya Jamii kutoka Kenya anasema,
“Ninashughulikia kina mama. Tulipatiwa mafunzo kuhusu lishe bora. Sasa natumia stadi nilizopata kuwafundisha kimamama kuhusu lishe bora na jinsi ya kulea mtoto, pamoja na umuhimu wa kumnyonyesha hadi afikie umri wa miezi 6, kisha kumwazisha lishe chenye virutubisho muhimu ili mtoto awe na afya bora”
Kando na usambazaji wa chakula kwa jamii, manusura pia hupokea msaada wa pesa taslim. Beatrice anasema fedha hizo zimemsaidia kukimu mahitaji mengine.
“Kuna pesa tulipata, ilitusaidia sababu tuna watoto wenye wanaendelea na masomo shuleni, na wadogo wenye wanahitaji kula vizuri. Pia hiyo pesa ilitusaidia kuanzisha biashara ili tuweze kujitegemea wenyewe bila kutegemea waume wetu.”
Na katika kaunti ya Homa Bay, Aida Achieng ni mmoja wa manusura wa mafuriko na pia mnufaika wa msaada wa jumla ya dola 91 sawa na shilingi Elfu 12 za Kenya kwa ajili ya lishe bora kwa watoto wake na jamii. Anasema,
“Ilikuwa ni wakati wa usiku wakati tulikuwa tumemaliza kula, saa ya kulala, ndipo maji yakaingia ndani ya nyumba kila mahali hadi mahali pa kulala. Kupitia UNICEF, nilipata $51 sawa shilingi 6,500 za Kenya, na baadaye tukapatiwa dola 40 (ksh. 5,500). Kwa vile nilikuwa kwa hali mbaya, ambayo kupata chakula ilikuwa shida na nilikuwa nalipa ada za shule, hizo pesa zilinisaidia sana. Nilichukua kidogo nikalipa ada za shule, kidogo nikanunua chakula na zingine nikaziweka ili kufanyia biashara. Ombi langu ni kuondoka pahali kama hapa ambapo mafuriko yanatuhamisha kila wakati, tunataka tuishi mahali hakuna kitu kitasumbua watoto, sasa naomba tu mungu atulinde”