
Ali Akbar Gharibshahi, bingwa wa mchezo wa kunyanyua vitu vizito wa Iran ameweka rekodi mpya ya dunia na kushinda medali ya dhahabu katika kategoria ya kilo wanamichezo wenye 107, kwenye Mashindano ya Dunia ya Kunyanyua Uzani ya 2025 nchini Misri.
Gharibshahi aliibuka kidedea kwa kunyanyua uzani wa kilo 255, na kuboresha rekodi yake mwenyewe ya dunia aliyoweka katika Michezo ya Walemavu ya 2024 huko Paris, aliponyanyua kilo 252.
Ingawaje alishindwa kunyanyua kilo 260 kwenye jaribio lake la mwisho, lakini umbuji wake kwenye raundi ya pili ulitosha kumpa medali ya dhahabu na kuweka rekodi mpya ya dunia.
Wanariadha kutoka mataifa 70 wanapambana kufa kupona kusaka medali tofauti, huku Misri ikiwa mwenyeji wa duru hiyo ya kwanza ya Mashindano ya Dunia ya Kunyanyua Uzani ya Walemavu (Para Powerlifting World).
Roohollah Rostami wa Iran (wanaume wasiozidi kilo 88), Amir Jafari (wanaume wenye kilo 72) na Mohsen Bakhtiar (wanaume wenye kilo 65) awali walikuwa wameshinda medali tatu za fedha katika mashindano hayo ya kimataifa.
Msururu endelevu wa Iran wa kuvunja rekodi na kuvuna medali lukuki umeifanya kuwa moja ya mataifa yenye mafanikio zaidi katika historia ya mchezo wa kuinua vyuma vizito.
Ushindi huo unaongeza idadi ya medali za Iran na kupiga jeki kasi ya timu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu, kabla ya maandalizi ya Michezo ya Walemavu ya 2028.