Baada ya kusitishwa mapigano na utawala wa Kizayuni, vikosi vya Muqawama vya Ghaza vimeingia katika vita vipya vya kupambana na magenge ya mamluki wa shirika la kijasusi la Israel Shin Bet kwenye Ukanda wa Ghaza ili kuwazuia majambazi hao kuunda maeneo yaliyojitenga chini ya uongozi wa utawala wa Kizayuni.

Vita vya Ghaza vimeanza kwa njia mpya baada ya usitishaji vita, na magenge yenye silaha yanayoungwa mkono na utawala wa Kizayuni yameingia katika vita dhidi ya vikosi vya Muqawama. Mashirika ya habari yameripoti kuwa, saa chache tu baada ya vikosi vya utawala vya Kizayuni kuondoka katikati ya makazi ya watu kwenye Ukanda wa Ghaza, magenge yenye silaha yanayoungwa mkono na Israel yaliuwa Wapalestina kadhaa na kuanzisha vita dhidi ya wanamapambano wa Muqawama ili kutumikia utawala katili wa Israel.

Utawala wa Kizayuni kupitia mashirika yake ya kijasusi unataka kuwagombanisha Wapalestina wa Ghaza ili kupata kile ambacho umeshindwa kukipata kwenye jinai zake za miaka miwili kwenye ukanda huo. Magenge hayo ya wanamgambo yaliyoundwa na Israel yanataka kuidhibiti Ghaza na kuiondoa HAMAS na makundi mengine ya Muqawama. Lakini katika siku za hivi karibuni, makundi ya Muqawama wa Kiislamu huko Ghaza yamepambana na mamluki hao wa Israel na kutoa kipigo kikali kwao. HAMAS imewataka wanachama wa magenge hayo ya kijambazi wanaojihusisha na magendo ya misaada ya kibinadamu, mauaji na jinai na baadaye kuisingizia HAMAS, wajisalimishe kwa vyombo vya usalama ndani ya wiki moja ili waweze kufikiriwa mustakbali wao la sivyo wajiandae na mkono wa chuma.

Kwa upande wake, Shlomi Diaz, mwandishi wa tovuti ya Kizayuni ya Hayom ameripoti kuwa, makundi yote ya Muqawama, ikiwa ni pamoja na Hamas, Jihadul Islamu na Popular Front, yanashiriki katika kampeni ya kupambana na magenge hayo ya mamluki wa Israel huko Ghaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *