Iringa. Waandishi wa habari mkoani Iringa wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha ulinzi na usalama wao, hasa wanaporipoti taarifa nyeti zinazohusu vitendo vya rushwa vinavyohusisha watu wa ngazi mbalimbali katika jamii.

Wito huo umetolewa Oktoba 17, 2025, katika semina iliyoandaliwa na Takukuru kwa waandishi wa habari wa mkoa huo, iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kipindi cha uchaguzi.

Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesema rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo kwani hupunguza uwajibikaji wa viongozi na wafanyabiashara, jambo linaloathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Rushwa ni adui wa haki na maendeleo. Inawajibika kwa kuzorotesha uchumi na kuzima sauti za wanyonge. Waandishi wa habari mnapaswa kutumia kalamu zenu kwa uadilifu, kuibua na kuripoti masuala yanayoathiri jamii badala ya kunyamazia vitendo vya rushwa,” amesema James.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, ni muhimu vyombo vya habari kuhakikisha usawa kwa vyama vyote vya siasa, huku wananchi wakihamasishwa kuchagua viongozi kwa uhuru bila kushawishiwa kwa njia zisizo halali.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Victor Swella amesema taasisi hiyo imeanza kampeni za kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uchaguzi safi na bila rushwa, ikiwa ni pamoja na kurusha vipindi vya elimu kupitia redio na televisheni.

“Tumeanzisha vipindi vya dakika 30 vya elimu kupitia vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa. Tunakutana nanyi leo kwa sababu tunaamini kalamu zenu zinaweza kubadilisha jamii. Kuzuia rushwa ni jukumu letu sote,” amesema Swella.

Awali, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard amebainisha changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya habari katika kuripoti masuala ya rushwa. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na hofu, vitisho, manyanyaso kazini, na ukosefu wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.

Waandishi wa habari mkoani Iringa kutoka vyombo vya habari tofautitofauti wakisiliza semina kuelekea uchaguzi iliyoandaliwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Iringa na kufanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa Manispaa ya Iringa.

Leonard amesema changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa waandishi kufuatilia kwa undani taarifa za rushwa, hivyo akaiomba Takukuru kushirikiana nao kwa karibu zaidi na kuhakikisha usalama wa waandishi unalindwa.

Kwa upande wao, baadhi ya waandishi walioshiriki semina hiyo waliitaka Takukuru kuonesha usawa katika kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa rushwa, bila kujali nafasi au hadhi ya mhusika.

“Tunahitaji kuona haki ikitendeka kwa wote. Si sahihi kuona mapapa wakifanya rushwa hawachukuliwi hatua, ilhali vidagaa wakikamatwa wanashughulikiwa haraka,” amesema Denis Mlowe, mwandishi wa habari kutoka Iringa.

Waandishi hao pia waliomba kujengewa uwezo zaidi wa kitaaluma na kisheria ili waweze kufanya habari za uchunguzi kwa usalama, uadilifu na weledi mkubwa, sambamba na kushirikishwa katika kampeni za kuelimisha umma juu ya mapambano dhidi ya rushwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *