
Simba haitakuwa na kipa wake chaguo la kwanza, Mousa Camara katika mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Nsingizini Hotspurs, Jumapili, Oktoba 19, 2025 huko Eswatini.
Kipa huyo tangu alipopata majeraha katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Gaborone United, bado hajarejea uwanjani na hivyo viatu vyake dhidi ya Nsingizini vitavaliwa na Yakoub Suleiman.
Benchi la ufundi la Simba limethibitisha kuwa Camara bado anauguza majeraha yake hivyo hatokuwepo katika mchezo huo wa keshokutwa Jumapili.
Mbali na Camara, Simba imethibitisha pia kuwa haitokuwa na kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber ambaye bado hajawa fiti baada ya kupona majeraha yake.
Meneja Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev amesema licha ya kuwakosa wachezaji hao, timu yake haina presha ugenini.
“Timu iko tayari kisaikolojia na kifizikia. Tunajua kwa nini tunaenda kule. Tunajua malengo yetu na tamanio letu ni kushinda mchezo. Tuna siku mbili za mazoezi kule kurekebisha vitu vidogo vidogo na kila kitu tunaamini kitaenda vizuri.
“Bajaber hatokuwa sehemu ya timu. Hajawa fiti kwa asilimia 100 hivyo hatuwezi kujiweka katika hatari kwa kumtumia tunamuacha arudi taratibu atakuwa sawa. Camara amepata majeraha hivyo hawezi kuwa sehemu ya timu,” amesema Pantev.
Ukiondoa wawili hao, Simba pia itaendelea kumkosa Abdulrazack Hamza ambaye tangu alipoumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, bado hajarejea uwanjani.
Simba tayari imeshaingia Eswatini jana jioni na leo itafanya mazoezi ya kwanza kujiandaa na mchezo huo.