Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Zuchu, 31, na yule wa Pop na RnB kutokea Marekani, Jennifer Lopez ‘J.Lo’, 56, wazo lao ni moja kuhusu tabia hasi za baadhi ya wanaume wakiwamo wale wanaowapenda, hivyo wameamua kuwa huru kuzungumzia hilo kwa mapana yake. 

Kupitia sanaa yao yenye ushawishi mkubwa, wanaieleza jamii yale wanayopitia na kile walichoamua baada kuona mambo yanaenda ndivyo sivyo sehemu waliyopaswa kupendwa na kuheshimiwa kama wanawake.

Zuchu, mwanzilishi Good People Gang (GPG), amefanya hivyo kupitia wimbo wake, Amanda (2025) unaovuma kwa sasa, huku J.Lo akitumia kibao chake, Ain’t Your Mama (2016).

ZU 01

Amanda ni wimbo unaozungumzia maumivu ya usaliti katika uhusiano ukibeba kisa cha mwanamke aliyejitoa kwa upendo na uaminifu kwa mpenzi wake lakini anajikuta akisalitiwa kwa mwanamke aitwaye Amanda.

Kufuatia hilo, Zuchu anajitokeza kwa sura ya upendo, huzuni, hasira na kujiamini akitaka ukweli kutoka kwa mpenzi wake kuhusu uhusiano na Amanda. Hatua hii inaonyesha jinsi alivyoumizwa ila bado anasimama kwa ujasiri bila kuficha maumivu yake.

ZU 02

Hivyo wimbo huu uliotengenezwa na S2kizzy na kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza, kwa ujumla unamhusu mwanamke aliyejeruhiwa kwa usaliti lakini anachagua kusema ukweli na kujikomboa kihisia.

Ikumbukwe, Amanda ulitoka baada ya Zuchu kuwa kimya kwa zaidi ya miezi sita akiipa nafasi ya kufanya vizuri albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) chini ya WCB Wasafi.

ZU 03

Ingawa kwa sehemu umekabiliwa na ukosolewaji mkali kutokana baadhi ya maneno yaliyotumika ndani yake, ila bado ni muziki mzuri unaoburudisha na kuchezeka. 

Kwa upande wa Ain’t Your Mama wake J.Lo, wimbo huu unamzungumzia mwanamke anayekataa kuwa mtumwa wa mapenzi au uhusiano usio na usawa kwa sehemu kubwa.

ZU 04

J.Lo anaeleza wazi kuwa hataki kuwa kama mama wa mpenzi wake, kwa kifupi hataki kufanya kazi zote za nyumbani kama kupika, kufua au kumtunza mwanaume ambaye hataki kuwajibika!

Lengo lake ni wa kuhimiza wanawake kuwa huru, kuthamini nafsi zao na kutokubali uhusiano unaowafanya watumike bila kuheshimiwa. Na pia unawakumbusha wanaume kuwajibika kwani mapenzi ni ushirikiano, si jukumu la upande mmoja.

ZU 05

Sasa ukisikiliza vizuri nyimbo hizo mbili (Amanda na Ain’t Your Mama), mwanzoni zinafanana kabisa kiujumbe ila mhusika mmoja anakataa yale anayoyalalamikia mwenzake kutoka kwa mpenzi wake.

“I cook and I clean… (napika na kufanya usafi…)” anaimba Zuchu. Lakini licha ya kumfanyia mwanaume wake yote hayo, bado jamaa anaenda kwa mchepuko wake ambaye ni Amanda.

ZU 06

Ndicho anachokikataa J.Lo katika wimbo wake huo chini ya Epic Records ambao hadi sasa video yake katika mtandao wa YouTube imetazamwa zaidi ya mara milioni 923 ikiwa ni miaka tisa tangu kuachiwa kwake.

“I ain’t gon’ be cooking all day, I ain’t your mama. I ain’t gon’ do your laundry, I ain’t your mama… (Sitatumia siku nzima kupika, mimi si mama yako. Sitakufulia nguo, mimi si mama yako…)” anaimba J.Lo.

Mtandao wa Rap-Up uliutaja wimbo huo kama msimamo wa kibabe sana, huku Jarida la Entertainment Weekly likieleza kuwa unapigania uhuru wa mwanamke kwa kupiga vita wapenzi wanaokuwa tegemezi kupita kiasi.

Kwa ujumla, J.Lo na Zuchu, wamelenga kuwapa nguvu mwanamke (female empowerment) – kujiamini na kutambua thamani yao, na pia kuwakumbusha wanaume kuwajibika katika majukumu yao na hata pale wanapofanya makosa.

“Unaweza kuwa na mshauri mzuri, rafiki mzuri mwenye upendo maishani mwako ambaye hukupa ujasiri na kukufanya ujisikie vizuri. Na hiyo ni nzuri sana, lakini mwisho wa siku ikiwa hujiamini, hayo yote ni sawa na bure,” anaeleza J.Lo.

Staa huyo baada ya kupata umaarufu kupitia filamu kadhaa ikiwamo Anaconda (1997), ndipo akageukia muziki akitoa albamu, On the 6 (1999) iliyokuwa na wimbo (If You Had My Love) ulioshika nafasi ya kwanza chati ya Billboard Hot 100.

Anachukuliwa kuwa mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa na waliochangia kukuza muziki wa Latin Pop, na pia alisaidia kuvunja vikwazo vilivyowakabili Wamarekani wenye asili ya Kihispania katika soko la Hollywood.

Mkali huyo wa kibao, On The Floor (2011) akimshirikisha rapa Pitbull, mwishoni mwa miaka ya 1990, alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa na albamu ya muziki na filamu zilizoshika namba moja nchini Marekani kwa wakati mmoja! Na unaambiwa alikuwa dansa wa Janeth Jackson hadi alidansi katika video ya wimbo ‘Thats The Way Love Goes’ wa Janeth.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *