
Dar es Salaam. Azam FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar dhidi ya KMKM leo, Jumamosi, Oktoba 18, 2025.
Matokeo hayo yanaifanya Azam ihitaji ushindi au sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano mwishoni mwa wiki ijayo ili itinge kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Azam pia inaweza kusonga mbele hata kama isiposhinda au kutoka sare lakini ni iwapo itapoteza kwa utofauti wa bao moja.
Azam imeonyesha mapema shauku ya kupata ushindi katika mchezo wa jana na hilo lilijidhihirisha katika dakika ya sita ilipopata bao la utangulizi kupitia kwa Jephte Kitambala.
Kitambala amefunga bao hilo kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia vyema pasi ya Yahya Zayd ambapo mshambuliaji huyo kutoka DR Congo aliupiga mpira kwa mtindo wa kuuzungusha upande wa kushoto wa kipa wa KMKM, Nassor Abdullah na kujaa wavuni.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Azam FC iliendelea kutawala mchezo na kuishambulia mara kwa mara KMKM na juhudi zao zikazaa matunda katika dakika ya 42 ilipopata bao la pili kupitia kwa Pascal Msindo.
Msindo amefunga bao hilo kwa mkwaju wa faulo aliouchonga moja kwa moja langoni mwa KMKM ambao ulimshinda kipa Abdullah na kutinga kimiani.
Hadi filimbi ya kumaliza kipindi cha kwanza ilipopulizwa, Azam FC ilienda katika vyumba vya kubadilishia nguo ikiwa mbele kwa bao 2-0.
Kipindi cha pili, KMKM walionekana kubadilika na kuidhibiti vyema Azam jambo lililofanya ubao wa matokeo kutobadilika hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Kikosi cha KMKM kilichoanza katika mchezo wa jana kiliundwa na wachezaji Nassor Abdullah, Ahmed Isihaka, Arafat Farid, Mohamed Ali, Firdaus Seif, Imran Mohamed, Jasper Yaw, Isihaka Said, Haji Makame, Mukea Allen na Mzee Hassan.
Kwa upande wa Azam FC, wachezaji walioanza ni Issa Fofana, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Landry Zouzou, Yahya Zayd, Abdul Seleman, Himid Mao, Jephte Kitambala, Feisal Salum na Idd Seleman.
Katika Uwanja wa Bingu jijini Lilongwe Malawi, Yanga imekutana na mshtuko wa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji wao Silver Strikers.
Bao pekee la Silver Strikers katika mchezo huo limefungwa Yosefe Andrew katika dakika ya 76 ya mchezo.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, Yanga bado ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwani inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao mawili katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumamosi ijayo ili itinge hatua ya makundi.