
Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema katika barua rasmi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kiduru wa Baraza la Usalama Vassily Nebenzia kwamba muda wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama unamalizika leo tarehe 18 Oktoba 2025.
Katika barua hiyo, Araqchi ameashiria vipengee vilivyo wazi vya azimio nambari 2231 na kusisitiza kuwa, suala la miradi ya nyuklia ya Iran linapaswa kuondolewa katika ajenda za Baraza la Usalama baada ya miaka kumi na kwamba kuanzia sasa hakuna msingi wowote wa kisheria wa kuwekea vikwazo mpango wa nyuklia wa Iran.
Katika sehemu ya barua yake, akikumbusha kupasishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2015, aliandika kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifungamana na mapatano hayo kwa nia njema tangu mwanzo na ndani ya fremu ya majukumu yake, lakini Marekani imefanya “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa” kwa kujiondoa kwa upande mmoja katika JCPOA na kurejesha vikwazo vyake mwaka 20.
Araqchi aidha amekosoa mienendo ya nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa JCPOA na kusema kuwa, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza si tu hazikutekeleza ahadi zao bali pia ziliweka vikwazo vipya dhidi ya Iran na hivyo kuyadhoofisha zaidi mapatano ya JCPOA.
Mapema leo pia Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ilitoa tamko kuhusiana na kumalizika muda wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran vinamalizika leo Jumamosi Oktoba 18, 2025.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ilieleza kwamba, baada ya kumalizika Azimio nambari 2231, mpango wa nyuklia wa Iran unapaswa kuhesabiwa kuwa ni mpango wa nyuklia wa amani kama ulivyo wa nchi yoyote isiyo ya silaha za nyuklia kwenye Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.