
Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza, ambacho kwa muda mrefu kinajulikana kama kilele cha elimu duniani, kinachunguzwa vikali baada ya kubainika wazi kwamba kimefanya uwekezaji kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika makampuni yasiyopungua 49 yanayojihusisha na vitendo haramu vya Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Tovuti ya habari na uchambuzi ya The Middle East Eye (MEE) imeripoti kuwa Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza kimewekeza zaidi ya pauni milioni 19 katika makampuni hayo yanayoshiriki katika shughuli haramu za Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Uchambuzi uliochapishwa juzi Alhamisi umeonyesha kuwa Chuo Kikuu cha Oxford kiliwekeza kupitia kile kinachojulikana kama “mfuko wa ufuatiliaji wa usawa ulioasisiwa mwaka 2020 na BlackRock, kampuni ya uwekezaji ya nchini Marekani, benki kubwa za Israel, kampuni za masuala ya usfairi kama Expedia, Booking.com, na Airbnb, na kampuni za teknolojia za Marekani kama Motorola Solutions.
Aghalabu ya kampuni hizo zimeorodheshwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa na haki za binadamu kuwa zimekuwa zikiuwezesha utawala wa Israel katika ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni.
Muungano wa Oxford BDS ambao ni kikundi cha wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho kikuu umekosoa uwekezaji uliofanywa na Oxford katika shughuli haramu za Israel katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kusema jambo hilo halikubaliki. Kikundi hicho cha wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Oxford wamesema kuwa ni jambo lilsilokubalika kwa chuo hicho kikuu kujihusisha na shughuli zozote haramu.