Dar es Salaam. Familia ya Tabu Msigala (49), ambaye mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, imeeleza  kutoweka nyumbani ndugu yao tangu Oktoba 13, 2025 saa 12 asubuhi, bila kuacha taarifa yoyote.

Msigala aliondoka nyumbani kwao bila kusema anakokwenda na familia haikuwa na wasiwasi licha ya kuondoka kwake asubuhi na hakuwa na simu.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 18, 2025, Rehema Msigala, dada yake Tabu, amesema siku ya tukio aliondoka na hakurudi tena, jambo ambalo si kawaida yake ya kuchelewa kurudi nyumbani.

“Ndugu yetu mara nyingi anakwenda kwa marafiki maeneo ya jirani lakini sio asubuhi kama siku hiyo alioondoka na hana tabia ya kuchelewa kurudi, mwisho wake ni saa 12 jioni, lakini siku hiyo hakurudi,” amesema Rehema.

Kwa mujibu wa Rehema, wameripoti kituo cha polisi cha Oysterbay na kupewa namba OUB/RB/ 7999/2025 na pia wametembea katika hospitali za mikoa yote mitatu pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Minazini, Makumbusho, Zunda Dogras amesema alipata taarifa za kupotea kwa Tabu kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

“Taarifa za kupotea kwa mtu huyo niliziona Facebook na nilimuuliza aliyeweka taarifa kama wamekwenda polisi akajibu ndiyo,” amesema Zunda.

Amesema kutokana na taarifa hizo amewaambia wananchi wake wasaidie kumtafuta kwa kutuma picha na maelezo maeneo mbalimbali ili kusaidia kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa Tabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *