KOCHA Mkuu wa Yanga, Romain Folz, amezungumzia kwa uchache sababu ya kipigo cha bao 1-0 ilichopokea timu hiyo leo Oktoba 18, 2025 kutoka kwa Silver Strikers huku kubwa zaidi akisema Jumamosi ya Oktoba 24, 2025 katika mechi ya marudiano, Wananchi watafurahi.

Yanga imepokea kipigo hicho katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi.

Katika mechi hiyo, bao lililoipa ushindi wenyeji lilifungwa dakika ya 76 na Andrew John aliyemalizia pasi ya Ernest Petro, huku Folz akisema kushindwa kwao kutumia vizuri nafasi ndiyo imesababisha matokeo hayo.

Shambulizi la bao hilo lilikuwa na pasi nne pekee, ambapo lilianzishwa na kipa George Chikooka, mpira ukaenda kwa beki wa kulia McDonald Lameck ambaye alimpasia kiungo wa kati Uchizi Vunga aliyeukokota mpira kwa muda mrefu hadi amekaribia boksi la Yanga, ndipo akamuachia Ernest Petro aliyempa pasi mfungaji Andrew Joseph na kumuacha kipa wa Yanga, Djigui Diarra na mabeki wake, Dickson Job na Ibrahim Bacca washindwe la kufanya.

Alipoulizwa kama mchezo ulikuwa mgumu, Folz amesema: “Siyo sana. Tunachohitaji ni kutumia vizuri nafasi tunazopata.”

Folz ambaye ameiongoza Yanga kucheza mechi sita za mashindano na kikosi chake kufunga mabao tisa huku kikiruhusu moja pekee, imeshuhudiwa timu hiyo mechi mbili za mwisho ikiondoka bila bao jambo ambalo kocha huyo amesema: “Tutayapata katika mchezo ujao Jumamosi.”

Kuhusu wapi wapinzani wao walikuwa bora kiasi cha kuifanya Yanga kupoteza, Folz amesema: “Nafikiri tulikuwa wabaya katika kumalizia nafasi zetu, lakini tutaboresha hilo na tutafanya vizuri Jumamosi.”

Yanga iliyoanza maandalizi ya mechi hiyo Oktoba 6, 2025, mastaa waliokosekana kambini kutokana na majukumu ya timu zao za taifa ni Duke Abuya (Kenya), Pacome Zouzoua (Ivory Coast), Prince Dube (Zimbabwe), Celestin Ecua na Lassine Kouma (wote Chad). Pia Israel Mwenda, Ibrahim Bacca, Offen Chikola na Bakari Mwamnyeto waliokuwa na kikosi cha Tanzania. Pia Dickson Job na Aziz Andabwile walikuwa na kikosi cha Tanzania, kabla ya kurejea kambini Yanga baada ya mechi ya kwanza ya Zambia iliyochezwa Oktoba 8, 2025.

Kukosekana kwa wachezaji hao ambao wengi walijiunga na wenzao siku chache kabla ya mechi ya leo, Folz amesema hilo haliwezi kuwa sababu ya wao kutocheza vizuri leo kwani hali hiyo itatokea msimu mzima kwani Kalenda ya FIFA itaendelea kuwepo.

Mfaransa huyo akamalizia kwa kuwaambia mashabiki wa Yanga ambao wamechukizwa na matokeo ya mechi ya leo, kwamba wasijali Jumamosi watafurahia.

Kipigo hicho kinaifanya Yanga kuwa na deni la kupata ushindi wa kuanzia angalau tofauti ya mabao 2-0 katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumamosi ya Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ili ifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kufanya hivyo 2023-2024 ilipofika hadi robo fainali ikinolewa na Miguel Gamondi na 2024-2025 ambapo Gamondi tena aliivusha lakini ikikwamia makundi kijiti alipoachiwa Sead Ramovic.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *