#HABARI: Mradi wa pamoja ya Vyama Vikuu vya Ushirika vya Korosho nchini (KCJE LTD), imekuja na mpango maalum wa kutatua changamoto ya muda mrefu inayowakabili wakulima na vyama vya ushirika kuhusu usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani hadi sokoni.
Akizungumza wakati wa ziara ya wajumbe wa mradi huo waliotembelea Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (Nyanza Cooperative Union), Kaimu Mtendaji Mkuu wa KCJE LTD, Mabruk Mpangule, amesema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya taasisi hiyo kwa mwaka huu ni kuhakikisha changamoto ya usafirishaji wa mazao kwa wanachama wake inapatiwa suluhisho la kudumu.
Amesema KCJE LTD imebaini kuwa changamoto hiyo imekuwa ikisababisha ucheleweshaji wa usambazaji wa mazao, ongezeko la gharama za uendeshaji na upotevu wa kipato kwa wakulima.
Amesema KCJE LTD imeweka mpango mahususi wa kununua malori 30 ambayo yatatumika kusafirisha mazao ya wanachama kutoka maeneo ya uzalishaji hadi kwenye masoko Amefafanua kuwa mpango huo utaanza kutekelezwa muda mfupi ujao mara baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi na maandalizi ya kifedha.
Mpangule amesema mpango huo wa usafirishaji ni sehemu ya juhudi za KCJE LTD za kuimarisha huduma kwa wanachama wake na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa thamani wa mazao, hasa korosho.