#HABARI: Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa barabara kuu ya TANZAM kipande cha Igawa – Tunduma (Km 218) na Ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari, katika barabara hiyo eneo la Iboya Mkoani Songwe.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Mkoa wa Songwe ulikumbwa na changamoto kwenye baadhi ya Barabara kutokana na mvua za El-Nino katika Barabara ya Kamsamba inayounganisha mkoa huo na mkoa jirani wa Rukwa ambapo Bilioni 32 zilitolewa ili kuondoa changamoto ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino ikihusisha Daraja la Mpapa lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Mlowo – Kamsamba kwa shilingi bilioni 7, Daraja la Sange lenye mita 25 na barabara za maingilio kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.3, daraja la Kabalisi lenye urefu wa mita 40 na barabara za maingilio kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.7, na Ujenzi wa barabara ya Zege na kuchoronga milima kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8.8 ambapo mradi unatakelezwa na makandarasi wazawa ukiwa umefikia takribani asilimia 90 mpaka sasa.
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe Mhandisi Suleiman Bishanga amesema hayo tarehe 18 Octoba 2025 wakati akizungumza ofisini kwake kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Amesema kuwa mkoa wa Songwe una mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,034.71 ambapo kati ya hizo kilomita 257 ni Barabara za lami na Kilomita 810 ni barabara za changarawe, Amesema serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la Kamsamba lenye urefu wa mita 84 kwa gharama ya shilingi bilioni 17 na Daraja la Mpapa/Mkonko lenye urefu wa mita 60 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7 ambalo limefikia asilimia 90 likiwa linajengwa na mkandarasi mzawa ABEMULO.