
Israel imerejesha miili ya Wapalestina 15 huko Gaza siku ya Jumamosi, na kufanya idadi hiyo kufikia 135. Taarifa hizo zimethibitishwa na wizara ya afya katika eneo linaloongozwa na Hamas.
Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump, Israel ilipaswa kukabidhi miili ya Wapalestina 15 kwa kila mwili mmoja wa Muisraeli aliyefariki utakaporejeshwa. Hamas ilikabidhi mwili wa mateka mwingine wa Israel siku ya Ijumaa.
Tangu usitishaji mapigano ulipoanza, Hamas imekabidhi miili ya Waisraeli tisa na mwanafunzi mmoja wa Nepal. Wizara ya afya ya Gaza ilisema kuwa baadhi ya miili iliyorejeshwa Jumamosi ilikuwa na dalili za unyanyasaji, kupigwa, kufungwa pingu na kufungwa macho. Jeshi la Israel limesema madai haya ni propaganda za uongo za Hamas.