Katavi. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi Oktoba 18, 2025, anatarajiwa kuendelea na kampeni za uchaguzi kunadi ilani ya chama hicho katika mikoa ya Katavi na Rukwa.

Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa kufanya mikutano mitatu ya kampeni katika mikoa hiyo.

Mikutano hiyo itatanguliwa na mkutano mkubwa utakaofanyika Mpanda mjini, ukifuatiwa na mingine miwili itakayofanyika Kibaoni (Mpimbwe) mkoani Katavi na Namanyere (Nkasi) mkoani Rukwa.

Mgombea huyo anatarajiwa kuendelea na kampeni zake leo baada ya kuhitimisha ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, akimalizia katika Mkoa wa Kagera.

Kanda ya Ziwa yenye jumla ya wapigakura 9,311,982 ni ngome ya chama hicho na Samia alianzia kampeni zake mkoani Mwanza Oktoba 7, 2025 baada ya kuhitimisha kampeni hizo katika mikoa ya Kaskazini.

Mikutano hiyo iliyokuwa ikihudhuriwa na maelfu ya wananchi ambapo kwa Kanda ya Ziwa, alifanya mikutano katika mikoa yote sita ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Geita na Kagera.

Akiwa katika mikoa hiyo, mgombea huyo, pamoja na masuala mengine, alitoa ahadi mbalimbali zinazolenga kuchechemua uchumi na biashara.

Samia alitoa ahadi akitilia mkazo katika shughuli za ujenzi wa viwanda, kuboresha miundombinu ya usafiri, kuendeleza sekta ya kilimo, madini, uvuvi, utalii pamoja na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, maji na umeme.

Katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji katika Kanda ya Ziwa ambayo ni kitovu cha biashara na usafirishaji wa ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Victoria na mipaka ya Kenya na Ugansa, Samia aliahidi kuboresha viwanja vya ndege vya Mwanza na Chato.

Mbali na uboreshaji wa viwanja hivyo viwili, pia ameahidi kujenga vipya vya Geita Mjini, Mugumu (Serengeti) pamoja na Missenyi (Kagera) ambavyo vitasaidia kukuza utalii na usafiri wa biashara.

Kwa ujumla ahadi za mgombea huyo Kanda ya Ziwa zimejikita katika kuunganisha sekta za uzalishaji (kilimo, madini, uvuvi na utalii) miundombinu ya viwanda na usafiri ili kujenga uchumi shirikishi.

Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28, 2025 na zitahitimishwa Oktoba 28 ambapo Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), idadi ya Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura ni 37,647,235 ambao wataamua nani awe diwani, mbunge na Rais.

Kwa mujibu wa taarifa ya INEC iliyotolewa Oktoba 7, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima orodha hiyo inaonyesha wapigakura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na 996,303 wapo Zanzibar.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa jumla ya vituo vya kupigia kura 99,895 vitatumika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *