
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Fergus Walsh
- Nafasi, Mhariri
Utafiti mpya umeonyesha kwamba kipimo cha damu kinachoweza kugundua zaidi ya aina 50 za saratani kinaweza kusaidia utambuzi wa ugonjwa huo kwa haraka zaidi.
Matokeo ya jaribio lililofanyika Amerika Kaskazini yanaonyesha kwamba kipimo hicho kiliweza kubaini aina mbalimbali za saratani, ambapo robo tatu kati ya hizo hazina aina yoyote ya mpango wa uchunguzi wa kuzitambua.
Zaidi ya nusu ya saratani hizo zilipatikana katika hatua za awali, ambapo ni rahisi zaidi kutibu na kuna uwezekano mkubwa wa kupona kabisa.
Kipimo cha Galleri, kilichotengenezwa na kampuni ya dawa ya Marekani iitwayo Grail, kinaweza kubaini vipande vya DNA ya saratani ambavyo vimejitenga kutoka kwenye uvimbe na kusambaa kwenye damu. Kwa sasa, kipimo hicho kinajaribiwa na Huduma ya Afya ya Taifa (NHS) nchini Uingereza.
Jaribio hilo lilihusisha watu wazima 25,000 kutoka Marekani na Canada kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo karibu mtu mmoja kati ya watu 100 alipata matokeo chanya. Kati ya visa hivyo, asilimia 62 vilithibitishwa kuwa na saratani baadaye.
Mtafiti mkuu, Dkt. Nima Nabavizadeh, ambaye ni profesa msaidizi wa tiba ya mionzi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Oregon, alisema kuwa takwimu zilionyesha kwamba kipimo hicho kinaweza “kubadilisha kwa kiasi kikubwa” mbinu yao ya uchunguzi wa saratani.
Alifafanua kwamba kipimo hicho kinaweza kusaidia kugundua aina nyingi za saratani “mapema, wakati ambapo kuna nafasi kubwa ya matibabu kufanikiwa au hata kupona kabisa.
Kipimo hicho kilitoa matokeo sahihi ya kutokuwa na saratani kwa zaidi ya 99% ya watu waliopata majibu hasi.
Kilipotumika pamoja na uchunguzi wa saratani ya matiti, utumbo mpana na shingo ya kizazi, kiliongeza jumla ya idadi ya saratani zilizogunduliwa mara saba zaidi.
Cha muhimu ni kwamba robo tatu ya saratani zilizogunduliwa zilikuwa ni zile ambazo hazina mpango maalum wa uchunguzi, kama vile saratani ya ovari, ini, tumbo, kibofu cha mkojo na kongosho.
Kipimo cha damu kilitambua kwa usahihi chanzo cha saratani katika visa tisa kati ya kumi.
Matokeo haya ya kuvutia yanapendekeza kwamba kipimo hiki cha damu kinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kugundua saratani mapema.
Lakini wanasayansi ambao hawakuhusishwa na utafiti huo wanasema ushahidi zaidi unahitajika kuonyesha kama kipimo hiki cha damu kinapunguza vifo vitokanavyo na saratani.
Clare Turnbull, profesa wa utafiti wa vinasaba vya saratani unaolenga kutumia matokeo ya utafiti wa maabara katika kuboresha uchunguzi, matibabu, au mbinu za kuzuia saratani, London, alisema: “Takwimu kutoka kwa tafiti za nasibu, zenye lengo la kupima viwango vya vifo, zitakuwa muhimu sana kubaini kama utambuzi wa awali wa saratani unaofanywa na kipimo cha Galleri kweli unasaidia katika kupunguza vifo.”
Matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa katika mkutano wa Jumuiya ya Ulaya ya Tiba ya Saratani (European Society for Medical Oncology) utakaofanyika mjini Berlin siku ya Jumamosi, lakini maelezo kamili bado hayajachapishwa katika jarida lililopitiwa na wataalamu wenzao (peer-reviewed journal).
Mambo mengi yatategemea matokeo ya utafiti wa miaka mitatu unaowahusisha wagonjwa 140,000 wa Huduma ya Kitaifa ya Afya (NHS) nchini Uingereza, ambao matokeo yake yanatarajiwa kuchapishwa mwakani, 2026.
Taasisi ya Huduma ya Kitaifa ya Afya (NHS) hapo awali ilisema kwamba endapo matokeo yatakuwa mazuri, itapanua wigo wa upimaji huo na kuwahusisha watu wengine milioni moja.
Sir Harpal Kumar, rais wa idara ya dawa za kibayoteknolojia katika kampuni ya Grail, aliyataja matokeo hayo kuwa ni ya “kuvutia sana.”
Akizungumza na kipindi cha Today cha BBC Radio 4, alisema: “Watu wengi wanaofariki kutokana na saratani hufariki kwasababu tunagundua saratani zao zikiwa zimeshafika hatua mbaya sana.”
Aliongeza kuwa saratani nyingi hugunduliwa zikiwa “tayari zipo kwenye hatua ambayo sio nzuri,” akifafanua kuwa lengo ni “kugundua mapema zaidi, wakati bado tuna nafasi ya kutumia matibabu yenye ufanisi mkubwa na yenye uwezo wa kuponya kabisa.”
Hata hivyo, Naser Turabi kutoka Shirika la Utafiti wa Saratani Uingereza alionya kwamba utafiti zaidi unahitajika ili “kuepuka kugundua saratani ambazo huenda zisingesababisha madhara.”
Aliongeza kuwa, “Kamati ya Kitaifa ya Uchunguzi ya Uingereza itakuwa na jukumu muhimu katika kupitia ushahidi na kuamua kama vipimo hivi vinapaswa kutumika na Huduma ya Afya ya Taifa (NHS).”