
MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, wameanza vyema tiketi ya kuisaka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya leo Oktoba 18, 2025 kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo, KMKM.
Katika mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mabao ya Azam yamefungwa na mshambuliaji, Jephte Kitambala Bola dakika ya 6, baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa KMKM, Nassor Abdullah.
Wakati Kikosi hicho Maalumu cha Kuzuia Magendo kikipambana kusawazisha, kilijikuta kikipigwa bao la pili lililofungwa na beki wa kushoto wa Azam, Pascal Msindo aliyepiga ‘Fri-Kiki’ kali ya moja kwa moja na kuzama nyavuni mwa Mabaharia hao.
Katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili, inamfanya mshambuliaji nyota wa Azam kufunga bao lake la pili kwenye michuano hii, tangu ajiunge na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam msimu huu akitokea, AS Maniema ya kwao DR Congo.
Nyota huyo alianza kufunga bao la kwanza katika mechi ya awali wakati Azam ilipoifunga El Merreikh Bentiu ya Sudan mabao 2-0, huku lingine likifungwa na Feisal Salum ‘Fei ‘Toto’, mechi iliyopigwa Septemba 20, 2025 kwenye Uwanja wa Taifa wa Juba, huko Sudan Kusini.
Katika mechi ya leo, Azam ikiongozwa na mkongwe, Himid Mao kwenye eneo la kiungo, ilionekana kuipa shida zaidi KMKM, ambayo muda mwingi ilikuwa ikicheza kwa tahadhari ya kujilinda, licha ya kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza.
Ushindi kwa Azam unaifanya timu hiyo kujitengenezea mazingira mazuri katika mechi ya marudiano itakayopigwa Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, ambapo inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuandika rekodi mpya.
KMKM imefika raundi ya pili ya michuano ya CAF baada ya kuitoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo mechi zote mbili baina ya timu hizo zilichezwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, huku kwa upande wa Azam ikiitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, ambapo kwa sasa inasaka rekodi ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo msimu huu.
Kikosi cha KMKM kilichoanza: Nassor ‘Cholo’ Abdullah, Ahmed Is-haka, Arafat Farid, Mohamed Ali, Firdaus Seif, Imran Mohamed, Jasper Yaw, Is-haka Said, Haji Makame, Mukea Allen, Mzee Hassan.
Kikosi cha Azam FC kilichoanza: Issa Fofana, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Landry Zouzou, Yahya Zayd, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Himid Mao, Jephte Kitambala Bola, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Idd Seleman ‘Nado’.