Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa ikitangaza kumalizika muda wa Azimio nambari 2231.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kumalizika muda wa Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema: Kama ilivyoelezwa katika misimamo na taarifa rasmi zilizopita kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la tarehe 20 Julai 2015 kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, kipindi cha miaka 10 kilichoainishwa kwa mujibu wa azimio hilo kinafikia tamati Jumamosi tarehe 18 Oktoba 2015, na vifungu vyake, ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, vitakomeshwa kuanzia tarehe hiyo.

Kwa mingi huo, suala la nyuklia la Iran, ambalo limekuwa kwenye ajenda za Baraza la Usalama chini ya kifungu cha “kutoeneza silaha,” linapaswa kuondolewa katika orodha ya masuala ya kujadiliwa na Baraza la Usalama. Vilevile harakati za kihasama za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, kama wavunjaji wa makubaliano ya JCPOA, ambazo, kwa nia ovu na bila kuzingatia taratibu husika za kisheria, zilitaka kurejesha maazimio ya Baraza la Usalama yaliyokuwa yamefutwa, hazipaswi kuwa na thamani au athari yoyote ya kisheria au kiutendaji. Sekretarieti ya Baraza la Usalama la UN pia hairuhusiwi kuidhinisha na kutambua hatua isiyo halali ya nchi hizo tatu.

Taarifa hiyo inasema: Jamhuri ya Kiislamu inakutambua kuanzishwa upya mifumo ya vikwazo vya Baraza la Usalama, ikiwemo Kamati ya Vikwazo na Kundi la Wataalamu, kuwa ni kinyume cha sheria na inaona kuwa Sekretarieti ina wajibu wa kurekebisha tovuti ya Baraza la Usalama haraka iwezekanavyo kwa kuondoa madai hayo. Taarifa hiyo pia imezitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kutambua kwamba muda wa Azimio nambari 2231 umemalizika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Tangazo la Iran kuhusu kumalizika muda wa Azimio nambari 2231 limekaribishwa na kuungwa mkono na nchi nyingi duniani. Katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, (NAM) zaidi ya nchi wanachama 121 wa jumuiya hiyo zilisisitiza kuwa Azimio nambari 2231 linapaswa kumalizika tarehe 18 Oktoba 2025. Kwa upande mwingine, nchi 21 wanachama wa Kundi la Marafiki wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, zilitoa taarifa mjini New York, na kusema kuwa Azimio nambari 2231 litamalizika muda wake Oktoba 18 na kwamba nchi wananchi hazitakiwi kutekeleza vikwazo ambavyo vimerejeshwa kwa njia isiyo ya haki na kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Sheria na ya Kimataifa, suala la msingi ni kwamba vikwazo ambavyo nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zinadai kuwa vimerejeshwa kupitia utaratibu wa snapback havina mashiko ya kisheria, na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazipaswi kutekeleza vikwazo hivyo. Ameongeza kuwa: “Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia ilitoa tamko muhimu sana, na katika hatua nyingine, tarehe 18 Oktoba, nchi tatu za Iran, China na Russia kwa pamoja zitatuma barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama, kubainisha ukweli kwamba muda wa azimio hilo umemalizika, na kwamba nchi wananchi hazina wajibu wa kutekeleza maazimio ya vikwazo ya Baraza la Usalama yaliyokwisha muda wake.”

Hii ni wakati Umoja wa Ulaya, ukiungwa mkono kwa siri na waziwazi na Marekani, unasisitiza msimamo wake juu ya kutekelezwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ta Kiislamu kama matokeo ya kuanzishwa tena mfumo wa snapback.

Inaonekana kwamba lengo la Wamagharibi katika kurudisha maazimio ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na kupinga mapendekezo chanya ya Tehran ni kuzidisha mashinikizo yasiyo na kifani kwa Jamhuri ya Kiislamu kwa shabaha ya kuilazimisha Iran ikubali matakwa haramu ya Marekani na nchi za Ulaya kuhusiana na sera za Iran za nyuklia, makombora na masuala ya kieneo. Kwa hiyo, Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya, ili kujifungamanisha zaidi na Marekani katika kampeni ya vikwazo dhidi ya Iran, na pia ndani ya mfumo wa makabiliano na Russia na kwa nia ya kuiadhibu Tehran kwa uhusiano wake wa kijeshi na Moscow, wametumia suala hili kama chombo cha kuzidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kuanzisha utaratibu wa snapback na kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, Iran na nchi washirika zinatilia mkazo kuwa hatua hizo ni kinyume cha sheria na kwamba Troika ya Ulaya haina mamlaka ya kutumia JCPOA ikiwa ni pamoja na snapback, kwa sababu nchi hizo hazijatekeleza wajibu wao na zimekiuka kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *