Leo Oktoba 18, 2025, vijana kutoka mkoa wa Tanga wameshiriki katika matembezi ya amani kwa lengo la kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya, pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Matembezi hayo yalianzia katika viwanja vya Tanga urithi na kuhitimishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, ambako washiriki walishiriki pia katika zoezi la usafi wa mazingira kama sehemu ya mchango wao katika kuimarisha huduma za afya na kudumisha usafi katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, mmoja wa waandaaji wa matembezi hayo amesema kuwa shughuli hiyo imelenga kuwaonyesha wananchi namna ambavyo serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika uboreshaji wa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya.
Aidha vijana walitoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa amani na utulivu ili kuchagua viongozi watakaoiendeleza nchi, hususan katika maeneo ya msingi kama afya, elimu na ajira.
#StarTvUpdates