BAADA ya kufungwa mabao 2-1 na Pamba Jiji, benchi la ufundi la Mashujaa FC limesema kwa sasa akili yao inawaza namna ya kufanya vizuri katika mechi ijayo dhidi ya TRA United itakayochezwa Oktoba 22, 2025, huku likitoa tahadhari ya ugumu wa ligi.

Mashujaa ilipata kipigo hicho jana Ijumaa Oktoba 17, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kubaki na alama nne kwenye msimamo baada ya mechi nne, ikiwa imeshinda moja, sare moja na kupoteza mbili.

Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Charles Fredy, amesema licha ya kipigo hicho bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na wanajiandaa kwenda kucheza na TRA United (zamani Tabora United).

“Leo tuko hapa Mwanza tumepoteza mechi ina maana sasa hivi akili yetu iko Tabora tufanye vizuri tupate pointi tatu tufanikishe malengo tuliyopewa na uongozi.

“Mchezo wetu na Pamba ulikuwa wa kiufundi zaidi, kila timu ilionyesha inahitaji pointi tatu, tumefanya makosa am-bayo tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kwenda kufanya masahihisho ya madhaifu ya mchezo huu,” amesema Fredy.

Akizungumzia ugumu wanaokutana nao kwenye ligi, Fredy amesema kila timu imefanya usajili bora na ina kikosi ambacho kinaweza kushindana na kupata alama tatu katika uwanja wowote.

“Kweli timu zimejiandaa msimu huu ligi ni ngumu timu zimesajili na zimejipanga, mpaka sasa nikiziangalia timu zote zina uwezo wa kuchukua pointi sehemu yoyote bila kujali ni nyumbani au ugenini, ukikaa vibaya unaweza kujikuta unafan-ya vibaya, kwahiyo lazima tujiandae vizuri,” amesema kocha huyo.

Mashujaa ni miongoni mwa timu zenye wachezaji wazuri kwenye eneo la ushambuliaji linaloongozwa na Daniel Lyanga, Ismail Mgunda, Crispin Ngushi, Salum Kihimbwa na Seif Karihe, jambo ambalo Fredy amesema lina faida kwao na linawapa machaguo mengi kila mchezo.

“Tuna wachezaji wazuri wengi na tumefanya usajili, tumeongeza watu wengi lakini inategemea na mpango wa mechi husika, mfano leo (jana) kipindi cha kwanza tulikuwa na mpango mwingine na kipindi cha pili mwingine na tumefanya kila kitu kuanzia pembeni na ushambuliaji lakini Pamba walikuwa vizuri kwenye ulinzi tukakosa nafasi,” amesema Fredy.

Katika mechi nne za Ligi Kuu Bara ilizocheza Mashujaa, imefunga mabao matatu kupitia Mundhir Vuai (mshambuliaji), Idrisa Stambuli (kiungo) na Baraka Mtui (beki).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *