
YAOUNDE, CAMEROON. Staa wa Manchester United, Bryan Mbeumo ameripotiwa kumhamasisha mchezaji mwenzake wa Cameroon, Carlos Baleba waungane pamoja Old Trafford.
Kiungo wa Brighton, Baleba aliivutia Man United na kupelekewa ofa kadhaa kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini klabu yake iligoma kumpiga bei.
Man United bado inahitaji huduma ya Baleba na inaweza kufanya jaribio jingine la kutaka saini yake wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa.
Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba Mbeumo anafanya kazi ya kumshawishi Baleba wakati walipokutana kwenye timu ya taifa Cameroon.
Mbeumo ana miezi michache tu huko Old Trafford, lakini anaamini Man United ni mahali salama kwa mchezaji mwenzake huyo kwenda kucheza soka lake.