Marekani. Aliyekuwa meneja wa marehemu DMX, ambaye ni mjomba wake, Ray Copeland ameibuka na kudai kuwa wasanii na watu wa karibu na rapa huyo hawakutoa msaada wa kifedha wakati wa maandalizi ya mazishi yake!.

DXM aliyetoka na albamu yake, Dark and Hell Is Hot (1998), alifariki dunia Aprili 9, 2021 katika Hospitali ya White Plains, New York nchini Marekani alipokuwa amelazwa tangu Aprili 2 baada ya kuzidiwa.

Katika mahojiano na mtandao wa AllHipHop, Copeland amesema alipiga simu kwa marafiki na washirika mbalimbali wa DMX, akiwamo Swizz Beatz, Ruff Ryders, Steve Rifkind, na lebo ya Def Jam, lakini wote walidai hawana fedha.

“Wakati wa msiba wa DMX, nilipiga simu kwa kila mtu, kuanzia Ruff Ryders, Swizz Beatz, Steve Rifkind hadi Def Jam. Niliwaambia gharama itakavyokuwa ila kila mmoja alisema hana fedha. Nikakata simu na kusema, ‘Basi, nitaweka mambo sawa mwenyewe,” alisema Copeland.

Baada ya kukosa msaada huo, Copeland aliamua kubeba jukumu hilo na kuandaa hafla kubwa ya mazishi yaliyofanyika katika ukumbi wa Barclays Center jijini Brooklyn, New York.

Alifanikiwa kukusanya zaidi ya Dola150,000, wastani wa Sh367.5 milioni kwa msaada wa marafiki wachache, akiwamo Germaine Miller na wakili Ron Sweeney.

“Nawashukuru kwa mchango wao mkubwa, kama si Germaine Miller, nisingeweza kumzika mpwa wangu kama alivyostahili. Yeye ndiye aligharamia mazishi yote kwa sehemu kubwa akitoa Dola150,000,” alisema Copeland.

Copeland pia alimpongeza rapa Kanye West kwa mchango wake mkubwa, akisema ndiye alihusika kwa kila kitu kilichofanyika katika ukumbi wa Barclays Center.

Katika hatua nyingine, alikanusha madai ya lebo ya Def Jam Records iliyodai iligharamia mazishi yote. Copeland anasema lebo hiyo ilitoa Dola35,000 pekee, na sio kama walivyoeleza.  

“Def Jam walinipa Dola35,000 tu lakini baadaye wakaviambia vyombo vya habari kuwa wao ndio waligharamia mazishi yote, jambo ambalo si kweli hata kidogo,” alisema Copeland.

Copeland alisema anasikitishwa na ukimya wa watu waliokuwa wamefaidika na mafanikio ya DMX, akisema rapa huyo aliwasaidia wengi kufikia mafanikio makubwa ya kimuziki na kifedha.

“Mtu huyu alitufanya sote tuwe mamilionea,” alisema kwa huzuni. “Lakini nililazimika kupambana na familia yangu kuhakikisha mazishi yake yanafanyika. Nashukuru kwa watu wote waliompenda kwa dhati.”

Aliongeza kuwa alikaribia kufanya mazishi ya kifamilia pekee huko Bronxville, lakini alishawishiwa kufanya hafla kubwa ili mashabiki waweze kumuaga DMX kwa heshima.

“Nilitaka kufanya mazishi yawe ya familia tu huko Bronxville ila wakaniambia, ‘Ray, huwezi kufanya hivyo. Watu wanahitaji kumuaga.’ Hivyo nikaamua kuendelea na hafla hiyo kubwa,” alisema.

Alikiri kuwa DMX hakuwa na bima ya maisha, jambo lililoongeza ugumu wa kugharamia mazishi yake. Licha ya watu wengi kutuma salamu za rambirambi mitandaoni, hawakuchangia chochote walipotakiwa kusaidia! 

Copeland ambaye alifanya kazi kama askari magereza, na kuja kumsaidia DMX katika hatua za mwanzo za muziki wake, alisema maneno ya marehemu kuhusu kutokuwa na marafiki katika tasnia ya muziki yalijidhihirisha baada ya kifo chake.

“Alikuwa akisema kila mara, ‘Sina marafiki kwenye tasnia ya muziki,’”. Na alikuwa sahihi. Alipofariki, ukweli huo ulionekana wazi kabisa,” alieleza Copeland.

Kipindi cha uhai wake, DMX alifanya vizuri na albamu zake mbalimbali na kuweka rekodi kadhaa ikiwamo ya kuwa msanii wa kwanza kutoa albamu na kushika namba moja mara tano mfululizo kwenye chati za Billboard Top 200.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *