Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa tamko kuhusiana na kumalizika muda wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Vizuizi vilivyowekwa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran vinamalizika leo Jumamosi Oktoba 18, 2025.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kwenye taarifa yake hiyo kwamba: Kama ilivyoelezwa katika misimamo na taarifa za awali za JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la tarehe 20 Julai 2015 kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, kipindi cha miaka 10 kilichoanzishwa chini ya azimio hilo kinamalizika leo Jumamosi, tarehe 18 Oktoba 2025, na vifungu vyake vyote, ikiwa ni pamoja na vikwazo vilivyotabiriwa ndani ya azimio hilo navyo vinamalizika leo.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: Suala la nyuklia la Iran, ambalo limekuwa kwenye ajenda ya Baraza la Usalama chini ya kichwa cha “kutoeneza”, linapaswa kuondolewa kwenye orodha ya vitu vinavyozingatiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baada ya kumalizika Azimio nambari 2231, mpango wa nyuklia wa Iran unapaswa kuhesabiwa kuwa ni mpango wa nyuklia wa amani kama ulivyo wa nchi yoyote isiyo ya silaha za nyuklia kwenye Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: Azimio nambari 2231 na kiambatisho chake, JCPOA, yalikuwa ni mafanikio makubwa ya diplomasia ya kimataifa ambayo yalionesha uaminifu na ufanisi wake katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwake. Kwa bahati mbaya, Merekani, ilijiondoa kinyume cha sheria kwenye makubaliano hayo mwaka 2018, na nchi tatu za Ulaya zikashindwa kutimiza majukumu yao, hazikuthamini mafanikio hayo muhimu ya kidiplomasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *