
Dar es Salaam. ‘Ledizi endi jentromeni’. Kama bado haujajua, dunia ya sasa siyo ya wachapakazi tu, bali ni dunia ya washawishi watu mitandaoni.
Unaitwa influencer ukiwa na followers elfu kumi tu. ukifikisha milioni moja, basi wewe ni ‘media house’ ya peke yako!
Huko mitandao kwao hujulikana kwa status kali, captions za moto na stori za kisirisiri. Wamegeuza simu zao kuwa benki halali. Yaani, unapiga post, unapata hela. Unatupa video hela inaingia. Ukipiga kelele wanakuja inbox wanakulipa.
Mchezo unachezwa mitandaoni. Ushawishi siku hizi ni biashara.
Kampuni, wanasiasa, NGOs na hata watu wa kawaida wanajua. Ukitaka stori yako isikike, tafuta mtu mwenye followers wengi.
Post moja inaweza kugharimu hadi mamilioni kama itakimbiza mitandaoni.
Lakini sasa, si wote wanaotumia nguvu hiyo kwa mambo ya maana. Wengine wameigeuza “silaha ya kidigitali.” Hutengeneza drama, skendo, au hoja kali kali zinazochochea mjadala. Siyo kwa mapenzi yao kwa nchi, bali kwa mapenzi yao kwa pesa.
Followers = Nguvu + Fedha. Kadiri unavyokuwa na likes nyingi, ndivyo watu wanavyoamini juu ya maneno yako. Wengine huandika post moja tu, lakini mitandao yote inachafuka! Na ukishaona watu wanagombana, kujibizana, au ku-share kila mahali, basi ujue “kazi imefika.”
Wapo wanaojifanya wanapigania haki, kumbe nyuma ya pazia kuna ‘sponsor’. Kaweka mkwanja ili wapige kelele kwa niaba yake.
Ni kama mchezo wa kisiasa wa kidigitali. Kila tweet inaweza kuwa kazi ya malipo. Hii ndiyo michezo ya influencers.
‘Biashara ya Ajenda’. Sasa, katika dunia hii ya digital hustle, kuna kitu kinaitwa “biashara ya ajenda.”
Hii ni pale ambapo mtu analipwa kusambaza taarifa, hata kama haina ukweli. Hawa hutumika sana kisiasa katika mataifa yao.
Wengine huambiwa wachafue jina la mtu, wengine wainue mtu fulani kisiasa. Hawa ni hatari sana haswa ukichukulia watu wetu wengi mabogasi, wanabeba lolote linalokuja na kuishi nalo. Ni upotoshaji wa kijamii.
Na kwa sababu wana wafuasi wengi wanaowaamini, kila kitu wanachosema kinaaminika haraka sana. Mitandao imekuwa kama “soko la habari zisizo rasmi.” kila mtu anauza “version” yake, ila tofauti ni kwa wengine huuza na risiti halali ya malipo!
Wafuasi wanapotea kwenye mchezo. Cha kusikitisha, kuna mashabiki wengi hawajui kama nyuma ya hashtags na “breaking news” nyingi, kuna pesa inapita.
Wanashiriki bila kujua wamekuwa sehemu ya biashara kubwa ya digital manipulation.
Wengine wanapigania hoja fulani wakidhani ni ya kizalendo, kumbe ni “kazi ya kulipwa” kutoka kwa mtu fulani. Yaani mtu anakaza shingo na komwe lake utadhani ana uchungu na nchi kumbe kamba, ni mpigaji wa pesa.
Kuna msemo mitaani unasema: “Kuna wanaopigania haki, na kuna wanaopigania hela kwa kutumia haki.” Nimesomeka vyema hapo ama nirudie tena? Kuna kupigania haki na kupigania pesa kupitia haki.
Influencers wa kizazi kipya. Sasa usiweke wote kwenye kapu moja.
Wapo wale wanaofanya kazi safi kabisa. Wanaelimisha, wanafanya biashara halali, wanaibua hoja na mijadala mizuri ya kijamii. Ndiyo!
Lakini pia, wapo waliogeuza mitandao kuwa soko la maneno, ukiwataka waseme, lipa kwanza. Hawa wanatumia mitandao kwa kazi chafu direct or indirect. Ni mapepo kama mapepo mengine. Siyo wanadamu safi.
Ushawishi ni nguvu, na nguvu hiyo ikitumiwa vibaya, inaweza kubadilisha nchi, maamuzi ya watu, au hata amani ya taifa.
Ni dunia mpya ya “vijana wenye simu, akili na followers.” Lakini hawana utu na uungwana.
Kwa kifupi. Mitandao imebadilika na kuwa ajira, jukwaa la siasa, na chanzo kikubwa cha hela. Lakini kama hujui kucheza mchezo huu kwa akili, unaweza kuwa mtumwa wa “likes” na “trending posts.” Na hili mifano ipo mingi ya waliobaki na likes na commentes bila pesa.
Na kama wewe ni mfuasi, usiamini kila anayeongea kwa sauti kubwa. Wengine wanapiga kelele kwa dau kubwa! Hulipwa, wanahongwa na kujazwa noti. Karibu katika dunia ya influencers ambapo kila post ni biashara, na kila kauli ina bei! Shituka.