Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz hapoi wala haboi kwa sasa mbele ya mashabiki wake kwa namna anavyotoa kazi mfululizo lakini ana malengo yake mawili nyuma ya pazia.

Ndani ya wiki mbili, Diamond ametoa nyimbo mbili, Msumari (2025) na Nani (2025), pamoja na video zake ambazo zimeonyesha ubunifu na ubora ukiwa ni utamaduni wake wa miaka mingi.

Cha kufurahisha ni kwamba nyimbo zote hizo ni za mahadhi ya Bongofleva, kitu ambacho ni mara chache kuona Diamond akifanya hivyo kutokana na dhamira yake ya kulishika soko la kimataifa.

Wimbo wake wa mwisho, Nani (2025), umekuja na hadithi ya mapenzi inayosimuliwa katika mazingira ya shule ambapo ameigiza kama mwalimu mwenye mvuto kwa wanafunzi, na anayejikuta akimpenda mwalimu mgeni.

Punde tu, penzi lao linachipuka kama inavyoonekana katika video yake ya inayozungumzia mapenzi, majaribu na uaminifu, huku ikiwa na ucheshi kutoka kwa wahusika wote.

Diamond anaeleza hisia zake kwa kusema hana sababu ya kutazama kwingine kwani mwanamke huyo ndiye kila kitu kwake. Kwa kujiamini, anakiri anavyochanganyikiwa hasa anapomwona amevaa na kupendeza.

Je, kwanini Diamond anaweka nguvu zaidi katika Bongofleva sasa?, mnamo Januari, staa huyo alisema mwaka huu ataachia albamu yake ya nne ambayo itakuwa ya muziki wa Bongofleva kwa asilimia kubwa.

Mwaka ndio huo unaelekea kuisha, kama atatimiza ahadi yake, basi hiyo itakuwa albamu ya kwanza tangu kuanza kufanya kazi na Warner Music Group (WMG), lebo kubwa duniani kutokea Marekani.

Mbali na nyimbo hizi mpya, hapo awali alishatoa Nitafanyaje (2025), Moyo (2025) na Kuna (2025), hivyo huwenda kazi zote hizo zikawa sehemu ya utangulizi wa albamu hiyo.

Tayari Diamond ametoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018), pamoja na Extended Playlist (EP) moja, First of All (2022).

Albamu zake mbili za mwanzo zote zilikuwa za Bongofeva ila ile ya tatu chini ya Universal Music Group (UMG), ililenga soko la kimataifa na ndio sababu ya kushirikisha wasanii wengi wa huko.

Miongoni mwao walioshirikishwa, ni P Square, Davido, Mr. Flavour na Tiwa Savage, wote kutokea Nigeria. Wengine ni Ne-Yo, Rick Ross na Omarion, wote kutokea Marekani.
Akiwa na miaka zaidi ya saba bila albamu mpya sokoni, bila shaka kiu yake ni kuona mashabiki wake wanapata kifurushi kipya cha burudani, nayo ni kutokea nyumbani, yaani Bongofleva.

Mnamo Julai, Diamond akiongea na Jarida la Billboard huko Marekani, alisema sababu zinazomfanya kuchukua muda mrefu bila kutoa albamu, ni tabia ya mashabiki kutozipa uzito sawa nyimbo zote zilizopo katika albamu.

“Siwezi kuweka nyimbo mbovu kwenye albamu yangu, lakini unapotoa albamu mara nyingine, inaua baadhi ya nyimbo kwa sababu watu wanataka wimbo mmoja tu ndio upewe kipaumbele,” alisema na kuongeza.

“Halafu nyimbo nyingine zinaonekana kama hazina maana, jambo ambalo nalichukia sana. Nadhani hiyo pia ni sababu iliyofanya nichukue muda kumaliza kazi hii,” Diamond alieleza.

Alisema anatumia muda mrefu kuandaa albamu ili watu wafurahie. Na sasa miaka zaidi ya saba bila kufanya hivyo ingawa EP yake ilikuwa na nyimbo nyingi, 10.

Mwaka uliopita, baadhi ya wasanii wa Bongofleva waliotoa albamu ni Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy) na Harmonize (Muziki wa Samia).

Wengine ni Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop), Marioo (The God Son), Rayvanny (The Big One), Zuchu (Peace and Money) n.k.

Sababu nyingine ambayo huenda inamsukuma Diamond kutoa nyimbo mfululizo, ni kufuatia majibizano yake na Mbosso mtandaoni miezi miwili iliyopita baada ya kuambiwa ana wivu na mafanikio ya msanii huyo.

Diamond alisema hawezi kuwa na wivu na Mbosso kwa kufanya vizuri na wimbo wa Bongofleva (Pawa) wakati yeye anazo kama hizo kibao zipo tu ndani na hajuli lini atazitoa maana anataka kuendelea kuvuma kimataifa.

Hivyo ni wazi anataka kudhihirisha kuwa bado anaweza kuifanya Bongofleva vizuri kuliko hata Mbosso ambaye alimsimamia chini ya WCB Wasafi kwa miaka saba.

Ikumbukwe EP ya Mbosso, Room Number 3 (2025) ambayo ni ya pili kutoka kwake, iliachiwa na nyimbo saba ambazo zimechanganya aina maarufu za muziki kama Bongofleva, Afrobeat, R&B na Amapiano. Nyimbo kutoka katika EP hiyo zilizofanya vizuri zaidi ni Pawa, Nusu Saa, Merijaah na Aviola.

Wanachosema wadau

Akizungumza na Mwananchi Belinda Maswa mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam anasema hatimaye Diamond kakumbuka mashabiki wake wa nyumbani.

“Yaani kama ile ‘Nani’ ni hatari sana sasa huyo ndiyo Simba ‘Diamond’ ambaye sisi tusiopenda Amapiano tulikuwa tunamkosa. Yani ameua ametuweza hasa, mimi natamani awe anatoa ngoma mfululuu za Bongo Fleva lakini ndiyo hivyo tena na yeye anafanya biashara,” anasema Belinda.

Naye Hamis Khalid mkazi wa Buguruni jijini humo anasema Diamond anataka kuonesha kuwa yeye ndiyo mwamba wa Bongo Fleva

“Unajua jamaa hapa katikati alituacha sasa sisi mashabiki wa ndani, ingawa kazi zake tulikuwa tunaziunga mkono, lakini hakuwa anatoa sana Bongo Fleva. Hii ndiyo ile ladha ya ‘Mbagala’ ule wimbo wake. Ukisikiliza kwa makini hizi nyimbo zake mbili unasikia kabisa fleva ya muziki mzuri,”anasema

Hata hivyo kwa upande wake George Edson anasema ni vizuri msanii huyo kukumbuka alipotoka.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *