Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama amemtaja aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, kuwa shujaa wa demokrasia ambaye alihimiza haki na usawa, si tu nchini Kenya bali pia katika bara zima la Afrika.
Kupitia ujumbe mtandaoni aliotuma salamau za rambirambi kwa Wakenya katika ukurasa wake wa Instagram leo Jumamosi, Oktoba 18, 2025, akiambatanisha na picha aliyopiga akiwa sambamba na mke wake, Michelle Obama, Raila Odinga na mkewe Ida Odinga.

Rais mstaafu huyo wa Marekani amemkumbuka Odinga kama mtoto wa harakati za kupigania uhuru, akisema baba yake Raila, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa miongoni mwa wapigania uhuru walioteswa na serikali ya kikoloni kwa kudai Kenya huru mwaka 1952.
“Mara kwa mara nilipokutana naye, nilishuhudia akitanguliza masilahi ya taifa kuliko matakwa yake binafsi. Kama viongozi wengine wachache duniani, alikuwa tayari kuchagua njia ya maridhiano na upatanisho hata baada ya nyakati ngumu,” amesema Obama katika ujumbe wake.
Obama, ambaye asili yake ni Kaunti ya Siaya ambako alizaliwa baba yake, Hussein Obama, amesema anamkumbuka Raila kwa mapokezi mazuri aliyompa alipofika Kenya kwa mara ya kwanza wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki, akiwa Seneta wa Jimbo la Illinois.

Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama (kushoto) akiwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Raila aliandamana na Obama hadi Kogelo, nyumbani kwa babu yake, ambako walimtembelea Sarah Obama.
“Maishani mwake, Raila alitoa mfano mkubwa wa uongozi siyo tu kwa Wakenya na Waafrika, bali kwa dunia nzima. Najua wengi watamkosa na kumkumbuka kwa dhati. Michelle na mimi tunatuma salamu za rambirambi kwa familia yake na wananchi wote wa Kenya,” amemalizia Obama.
Raila Odinga, aliyefariki dunia Oktoba 15, 2025 wakati akipatiwa matibabu nchini India, anatarajiwa kuzikwa kesho Jumapili nyumbani kwake Kisumu.