
BAADA ya leo Oktoba 18, 2025 kushuhudia Yanga ikipoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers huku Azam ikiichapa KMKM mabao 2-0, kesho Jumapili Oktoba 19, 2025 Simba na Singida Black Stars zitakuwa dimbani huku kila upande ukiingia kwa tahadhari, lakini kuna jambo wameahidi.
Timu hizo zinatupa karata zikiwa kwenye mataifa tofauti na michuano tofauti. Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na itakuwa mgeni wa Nsingizini Hotspurs nchini Eswatini kwenye Uwanja wa Somhlolo, wakati Dimba la Intwari pale Burundi, wenyeji Flambeau du Centre wataikaribisha Singida Black Stars ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi zote zitaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
PANTEV AAHIDI FURAHA
Simba iliyofundishwa na makocha wawili tofauti akianza Fadlu Davids kisha Hemed Suleiman ‘Morocco’, sasa inakwenda kukabiliana na Nsingizini Hotspurs huku benchi la ufundi likiwa na mabadiliko baada ya ujio wa Dimitar Pantev ambaye awali alikuwa Gaborone United, wapinzani walioondolewa na Simba hatua ya awali kwa jumla ya mabao 2-1.
Nsingizini Hotspurs msimu uliopita 2024-2025 wakati Simba ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, yenyewe iliishia hatua ya awali ya michuano hiyo ikiondolewa na Stellenbosch kwa jumla ya mabao 8-0, nyumbani ilifungwa 3-0 na ugenini ikachapwa 5-0. Stellenbosch ilipokutana na Simba hatua ya nusu fainali, ikapoteza kwa bao 1-0.
Nsingizini Hotspurs imepata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Eswatini msimu wa 2024-25 ikiwa chini ya kocha wa muda, Simon Ngomane, kwa sasa inafundishwa na Mandla David Qhogi.
Mara ya mwisho Simba kucheza nchini Eswatini ilikuwa Desemba 4, 2018 ikiifunga Mbabane Swallows mabao 4-0 kupitia Clatous Chama aliyetikisa nyavu mara mbili dakika ya 28 na 32, Emmanuel Okwi (dk 51), Meddie Kagere (dk 62). Jumla Simba iliiondosha Mbabane kwa mabao 8-1 baada ya mechi ya kwanza jijini Dar Wekundu hao wa Msimbazi kushinda 4-1, wafungaji wakiwa John Bocco dakika ya 8 na 33, Meddie Kagere (dk 84) na Clatous Chama (dk 90+1).
Kuelekea mechi ya kesho, Pantev, amesema: “Maandalizi yako kawaida, ingawa kidogo tofauti kwa sababu tunatumia uwanja wenye nyasi bandia, lakini timu iko tayari, imepata motisha ya kutosha na nafikiri lengo letu ni kutoa uwezo wetu wote, kucheza vizuri na kama nilivyosema awali, kila kitu kitategemea utendaji wetu. Hivyo tutafuata mbinu yetu tuliyojiandaa nayo.
“Hatutabadilisha chochote. Tuna mtindo wetu wa kucheza na tutacheza soka letu. Nafikiri kila kitu kitaenda sawa kwetu. Labda itakuwa ngumu kidogo kwa wachezaji wetu kwa sababu hapa kuna baridi sana, lakini huu ni mchezo wa mpira wa miguu, hali ni ile ile kwa sisi na kwa wao pia.”
Kwa upande wa Nsingizini Hotspurs kupitia rais wa klabu hiyo, Derrick Shiba, ametangaza kwa ujasiri kuwa hatma ya timu yao katika michuano hiyo itajulikana leo Jumapili.
Klabu hiyo yenye maskani yake Shiselweni, inayoongozwa na kocha raia wa Afrika Kusini, Mandla Qhogi, baada ya mechi ya kesho, itatua Dar es Salaam kurudiana na Simba Oktoba 26, 2025, mshindi wa jumla atapata nafasi ya kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Shiba alisisitiza umuhimu wa kufanya vizuri nyumbani akisema: “Kucheza vizuri ni jambo la msingi sana. Mchezo wetu wa kwanza utachezwa katika Uwanja wa Somhlolo, na huo ndiyo fainali yetu. Ni lazima tushinde na kuongoza nyumbani, kwa sababu kile kitakachotokea nchini Tanzania kitategemea matokeo ya mchezo wa kwanza.”
Kikosi cha Nsingizini kimepata nguvu mpya kufuatia kurejea kwa viungo watatu wa kati, Thubelihle Mavuso, Sizwe Khumalo na Neliswa Dlamini ambao awali walikuwa wameitwa kwenye kikosi cha taifa cha Eswatini.
Simba inapaswa kuwa makini na mshambuliaji Ayanda Gadlela na kiungo Sizwe Khumalo ambao wamekuwa wakifanya vizuri huku mara ya mwisho katika mechi ya kirafiki iliyochezwa hivi karibuni kati ambayo Nsingizini ilishinda mabao 2-1 dhidi ya timu ya Black Bulls kutoka Msumbiji, wote waliifungia timu yao mabao hayo muhimu.
‘TUTAMALIZANA DAR’
Rekodi inayosaka Singida Black Stars ni kama ile iliyowekwa na Namungo msimu wa 2020-2021 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi.
Singida Black Stars inafahamu kwamba zipo timu za Tanzania zilizowahi kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo na kushindwa kucheza makundi ambazo ni KMC (2019-2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021-2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025), lakini pia Azam iliyowahi kushiri-ki mara kadhaa.
Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, amesema: “Tumewaangalia wapinzani. Tumechambua mechi yao dhidi ya Al-Akhdar ya Libya, na pia tumeangalia baadhi ya mechi zao za ligi. Natarajia itakuwa mechi nzuri kwa sababu tuna kikosi kilichosawazika na wachezaji wenye uzoefu.
“Kwetu hii ni mechi muhimu kwa sababu ni hatua ya mwisho kabla ya kuingia makundi, siku zote nimekuwa nikisema tunatakiwa kucheza dakika 180 ili kufikia malengo, ambapo 90 za ugenini na zingine Dar es Salaam kitu ambacho ni ki-zuri kumalizia nyumbani.”
Singida Black Stars imefika hapo baada ya kuitoa Rayon Sports kwa mabao 3-1, ilianzia ugenini na kushinda bao 1-0, nyumbani ikashinda tena 2-1. Kwa upande wa Flambeau du Centre imeitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.
Flambeau du Centre, ilianza kushiriki mashindano ya kimataifa mwaka 2022, ilianza Ligi ya Mabingwa Afrika na mwaka huu inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika. Hivyo ni mara ya pili kimataifa.
Msimu wa 2022-2023 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, iliishia hatua ya pili ikitolewa na Zamalek kwa jumla ya mabao 6-1. Kabla ya hapo, hatua ya awali iliitoa Al Ittihad ya Libya kwa bao la ugenini baada ya sare ya 2-2.
Baada ya mechi ya leo, timu hizo zitarudiana wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla anafuzu makundi.