Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Cecilia Pareso amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kupiga kura kwa sababu ni haki yao, tendo la uzalendo na ndizo zinazoamua kupatikana kwa viongozi.
Katika kauli yake hiyo, amesema ni kosa kwa mtu yeyote kuwazuia wananchi kwenda kupiga kura, akirejea Kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Paresso ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 alipozungumza na wananchi wa Mpwapwa mkoani Dodoma katika mkutano wa kampeni za uchaguzi.

Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kwenda kupiga kura kwa sababu kufanya hivyo ni uzalendo, haki na wajibu na kunaamua kupatikana kwa viongozi watakaoongoza na kuleta maendeleo.
“Kupiga kura ni haki na wajibu wetu sisi ambao sheria inatutaka tujiandikishe na twende kupiga kura. Kupiga kura ni kujihakikishia maendeleo yako kwa miaka mitano ijayo,” amesema.
Amesema kura ndiyo inayounda Serikali yenye misingi imara ya kujenga ustawi wa wananchi na hatimaye uchumi kwa Taifa kwa ujumla.
Paresso aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, amesema ni kosa kwa yeyote kuwazuia wananchi kwenda kupiga kura.
“Kwa hiyo wanaowazuia watu wasiende kupiga kura, maana yake watakuwa wanatenda kosa na kwa namna yoyote ile sheria inachukua mkono wake,” amesema.

Kauli kama hiyo, ilitolewa pia na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima aliyesema ni kosa kisheria kuwazuia wananchi kwenda kupiga kura.
“Mtu yeyote au kwa niaba ya yeyote anayeshawishi watu wasiende kupiga kura, anatenda kosa kwa mujibu wa sheria hii. Mamlaka zinazohusika zitapitia kifungu hiki na zitashughulika na wanaohusika kufanya shughuli hizi,” amesema.
Katika msisitizo wake kuhusu hilo, amesema kitendo cha wananchi kuacha kwenda kupiga kura, kutasababisha uchaguliwe kiongozi usiyemtaka kwa mud awa miaka mitano.
“Uchaguzi wa Tanzania mtu hashindi kwa asilimia, anashinda kwa idadi ya kura, kura yako wewe ingeweza kumfanya usiyemtaka asiwe Rais, asiwe mbunge watu wajitokeze kupiga kura,” amesema.
Hata hivyo, amesema anadhani watu watajitokeza kwa wingi kwa sababu kampeni zimesfanyika katika mazingira mazuri na hazijahusisha purukushani.
Ameahidi ni matarajio yake ndani ya saa zisizozidi 72, INEC itakuwa imeshamtangaza mshindi wa kiti cha urais na makamu wa rais, kisha itaachia Serikali hatua zinazofuata.
Kifungu cha 129 cha sheria hiyo kinasema, “mtu ambaye kwa dhahiri au kwa kificho, yeye mwenyewe au mwingine kwa niaba yake, anatumia au kutishia kutumia, nguvu, vurugu au kuzuizi au anasababisha au anatishia kusababisha, yeye mwenyewe au mtu mwingine yoyote jeraha ya mwili au la kiroho, uharibifu, madhara.
“…au hasara au dhidi ya mpiga kura yeyote kumshawishi kupiga kura au kutokupiga kura, ikiwa mpigakura huyo, amepiga kura au ameacha kupiga kura katika uchaguzi wowote, au kwa kumteka nyara, vitisho au hila ya aina yoyote, kumkwamisha au kumzuia kupiga kura katika uchaguzi wowote, ametenda kosa la ushawishi mbaya kwa maana ya sheria hii,” kinaeleza kifungu hicho.
Katika mkutano huo, Paresso ameongeza CCM ndicho chama pekee kilichosimamisha wagombea wenye uwezo wa kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
Amesema ni CCM pekee ndicho chama kinachozijua shida na changamoto za wananchi na chenye uwezo wa kuzitatua kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030.